Jeshi la Polisi limepokea vifaa tiba kutoka shirika la Project Cure la nchini Marekani vyenye thamani ya Sh2 bilioni.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Siro akizungumza alipopokea vifaa hivyo katika Hospitali Kuu ya Polisi Kilwa Road leo Ijumaa Novemba 17,2017, amesema vitasambazwa katika vituo vya tiba vya polisi 20.
IGP Siro amesema wanalenga kuhakikisha askari wanapata huduma bora na kuwafanya wawe imara katika kutekeleza majukumu yao.
“Tutajitahidi kuwasomesha wataalamu wetu wa afya ili waweze kufanya kazi kwa weledi. Hospitali kuu ya polisi ipo vizuri, hivyo tunawakaribisha kwa yeyote atakayehitaji kutibiwa hapa kwa kuwa ina vifaa bora,” amesema IGP Siro.
Pia, amezindua majengo matatu katika hospitali hiyo ambayo ni kwa ajili ya wagonjwa mahututi, stoo kuu ya dawa na jengo la kuhifadhia maiti.
Kamanda wa Afya, Paul Kasabago amesema wanakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba katika wodi ya wagonjwa mahututi itakayofunguliwa.
Kasabago amesema wanahitaji mashine za CT- scan na MRI ili kuendelea kuboresha hospitali hiyo iweze kutimiza vigezo vya kuwa hospitali ya rufaa.
Ameishukuru Serikali ya watu wa Marekani kupitia shirika la misaada la USAID kwa kufadhili juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na Ukimwi kupitia shirika lisilo la kiserikali la JSI na AIDSfree Tanzania linalofanya kazi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika majeshi ya Polisi na Magereza.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la JSI, Peter Maro amesema mradi wa AIDSFree umetoa mafunzo kwa watumishi wa afya katika nyanja mbalimbali za utoaji wa huduma za Ukimwi na Kifua Kikuu.