Jeshi Lakanusha Kufanya Mapinduzi ya Kijeshi Zimbabwe Lasema Mugabe na Famia Yake Wapo Salama

Jeshi Lakanusha Kufanya Mapinduzi ya Kijeshi Zimbabwe Lasema Mugabe na Famia Yake Wapo Salama
Jeshi la Ulinzi la Zimbabwe limetupilia mbali uvumi ulioenea kupitia mitandao ya kijamii juu ya kufanyika mapinduzi nchini na limesisitiza Rais Robert Mugabe na familia yake wako salama.

"Kilichofanywa na vikosi vya ulinzi vya Zimbabwe ni kuleta amani kutokana na kushuka kwa hali ya kisiasa, jamii na uchumi nchini,” amesema msemaji wa jeshi katika matangazo ya moja kwa moja kupitia shirika la utangazaji la ZBC alfajiri leo.

"Kwa watu wote na ulimwengu nje ya mipaka yetu, tunapenda kuwafahamisha kwa uwazi kabisa kwamba serikali haijapinduliwa,” ameongeza.

Zimbabwe imekuwa katika hali ya sintofahamu baada ya jeshi kudaiwa kuteka majengo kadhaa ya serikali yakiwemo ya shirika la utangazaji la ZBC.

Mashuhuda walisikia milio ya milipuko maeneo mbalimbali ya jiji la Harare alfajiri hali iliyozidisha hofu katikati ya ripoti za kuwepo kutoelewana kati ya serikali ya Rais Robert Mugabe na vikosi vya ulinzi.

Vyombo vya habari vya hapa nchini vimeripoti kwamba jeshi limeteka majengo ya makao makuu ya ZBC.

Hata hivyo, msemaji wa jeshi amesema Rais Mugabe na familia yake “wako salama na wana afya njema na ulinzi wao ni wa uhakika.”

Shuhuda mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kwamba alisikia milio ya bunduki karibu na makazi binafsi ya Rais Mugabe alfajiri ya Jumatano.

"Kutoka kwenye uelekeo wa nyumba yake tumesikia milio ya bunduki 30 au 40 katika muda wa dakika tatu au nne majira ya saa 8:00 usiku,” mkazi mmoja wa jirani alinukuriwa akisema.

Pamoja na maelezo hayo, Jumanne watu walishuhudia magari ya kijeshi vikiwemo vifaru nje ya jiji la Harare, siku moja baada ya mkuu wa majeshi Jenerali Constantino Chiwenga kutishia kuingilia kati kukomesha ufukuzwaji kwenye chama cha Zanu PF na serikalini washirika wa Rais Mugabe.

Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini, Isaac Moyo, amepuuza uvumi wa mapinduzi dhidi ya utawala wa miaka 37 wa Rais Mugabe.

"Hakuna kitu kama hicho. Hayo ni madai ya kwenye mitandao ya kijamii,” Moyo aliliambia shirika la Reuters.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad