Rais Robert Mugabe aliyetawala Zimbabwe kwa miaka 37 amekamatwa na jeshi na kuwekwa kizuizini, chama tawala cha Zanu-PF kimesema.
Taarifa zinasema mawaziri kadhaa ambao wamekuwa wakitajwa kuwa ni “wahuni” na “wahalifu” wamekamatwa katika kile jeshi limeita ni “mapito yasiyo ya umwagaji damu.”
“Hakuna mapinduzi, ila kuna mapito yasiyo ya umwagaji damu ambapo baadhi ya mafisadi na wahuni wamekamatwa na mzee ambaye alitumika na mkewe kujinufaisha ametiwa ndani,” Zanu PF wamesema kupitia ujumbe wa Twitter.
“Milio kadhaa ambayo tuliisikia ilikuwa kutoka kwa wahuni ambao walikuwa wanagoma kukamatwa, lakini sasa wamewekwa ndani.”
Akaunti hiyo haikuwa imethibitishwa lakini si jambo la kawaida kwa ujumbe halali wa Twitter wenye uhusiano na serikali ya Zimbabwe na chama tawala kutothibitishwa na mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, maswali mengi yameibuka juu ya nani anayesimamia akaunti zenye uhusiano na chama tawala na kambi hasimu.
Chama tawala kimeonekana kutetea hatua ya Mugabe kuwekwa kizuizini kikisema ilikuwa lazima “kwa msingi wa Katiba na usafi wa taifa ".
Mugabe amewekwa kizuizini muda mfupi baada ya makamu wa rais aliyefutwa kazi wiki iliyopita Emmerson Mnangagwa kurejea nchini kutoka uhamishoni. Mnangagwa, ambaye alikimbilia Afrika Kusini amerejea asubuhi na kutua kwenye kambi ya Jeshi la Anga ya Manyame, limeandika gazeti la The Guardian.
Kuna fununua kwamba jeshi linaweza kumsimika jenerali huyo wa zamani kuwa mkuu wa serikali huku Mugabe akibaki mtu mwenye cheo asiye na mamlaka.
“Si Wazimbabwe wala Zanu-PF wanaomilikiwa na Mugabe na mkewe. Leo inaanza zama mpya na komredi Mnangagwa atatusaidia kuipa maendeleo Zimbabwe,” ulisema ujumbe mwingine wa Twitter.