HUKU watu mbalimbali wakiwemo maarufu nchini wakilia kuwa, hali ya uchumi siyo nzuri ‘vyuma vimekaza’, mwanadada anayefanya vizuri kwenye ulimwengu wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja ‘Kay’ hivi karibuni ameibua gumzo baada ya kumfanyia kufuru Kassim Mganga ambaye ni staa wa muziki wa Bongo Fleva.
Kufuru aliyoifanya Kajala ni ya kummwagia minoti Kassimu alipokuwa akitumbuiza kwenye shoo katika Ukumbi wa Next Door uliopo Masaki jiji Dar, kiasi cha kuibua gumzo kutoka kwa wahudhuriaji waliofika ukumbini hapo.
“Mh! Jamani kweli kwa watu wengine vyuma vimeachia, yaani kwenye hali kama hii mtu anaweza kumwaga minoti hivi? Kweli ukisema huna pesa, si kila mtu hana pia,” alisikika mwanadada mmoja aliyekuwa kwenye shoo hiyo.
Naye njemba mwingine ambaye alikuwa karibu na paparazi wetu alisikika akimwambia mtu aliyekuwa amekaa naye karibu kwamba: “Matukio ya watu kufanya kufuru kwa kumwaga noti siku hizi yamepungua
Na hata kwa ambao bado wanamwaga minoti, wengi ni wanawake tofauti na wanaume walivyokuwa wanafanya, labda kwa sababu wengi wao wanahongwa.” Hata hivyo, kwa Kajala maneno hayo ambayo watu mbalimbali walikuwa wakizungumza kutokana na tukio alilokuwa analifanya ni kama yalikuwa yanamhamasisha kuendelea kumfanyia kufuru Kassim kwani aliendelea kumdondoshea monoti huku mwanamuziki huyo akilitaja jina lake (Kajala).
Baada ya tukio hilo, mwandishi wetu alimtafuta Kajala ili aweze
kulizungumzia tukio hilo ambapo alifunguka; “Kiukweli Kassimu mimi alinikosha. Wimbo wake aliokuwa anauimba wa Somo ninaupenda sana na ndiyo maana sikuona shida kummwagia minoti. “Sifikirii kama ni kitu kibaya mtu kuonesha furaha yake, hasa sehemu za burudani kama hizo ambazo tunakwenda kwa ajili ya kuzifurahisha nafsi zetu.”
Kajala alipoulizwa alimmwagia mkali huyo wa Bongo Fleva kiasi gani cha fedha alisema kuwa, hakumbukuki maana hakuwa anahesabu na kuongeza kuwa kwake hilo ni suala la kawaida kabisa hasa akiwa amefurahishwa kwa kupewa kile ambacho moyo wake unapenda. “Pesa kama hivyo siwezi kuona shida kutoa pale ninapokuwa kwenye furaha zangu, ninatafuta kwa ajili ya kutumia na matumizi yenyewe ndiyo kama hayo,” alimaliza Kajala.
Chanzo Global Publishers