Kama ulisikia, hivi karibuni baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa, uongozi wa Yanga ulidaiwa kuwa katika harakati za kumuwinda kiungo mshambuliaji wa Simba, Mohammed Ibrahimu ‘Mo’.
Yanga ilifikia hatua hiyo baada kuona kiungo huyo mbunifu uwanjani hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Hata hivyo, baada ya Simba kupata taarifa hizo ilidai kuwa mchezaji huyo ambaye mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu haendi popote, lakini pia kocha mkuu wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog amepigilia msumari juu ya hilo kwa kusema kuwa Mo haondoki klabuni hapo.
Omog amesema kuwa Mo ni mmoja kati ya wachezaji anaowahitaji zaidi katika kikosi chake, kwa hiyo hayupo tayari kumuona akiondoka klabuni hapo.
“Kama kuna timu yoyote inamhitaji Mo kwa sasa hawezi kuondoka, bado tunamhitaji zaidi katika kikosi chetu na uongozi nimeshauambia juu ya hilo.
“Nilikuwa simtumii kwa sababu alikuwa ni majeruhi na sasa amepona, ndiyo maana unaona nimeanza kumtumia na matunda yake yanaonekana uwanjani, sipo tayari kuona akiondoka kikosini kwangu kwa sasa kama hao Yanga wanamtaka basi wasubiri lakini siyo sasa,” alisema Omog.