Kichuya Afunguka Kuhusu Mkataba Wake wa Simba

Kichuya Afunguka Kuhusu Mkataba Wake wa Simba
HUKU mkataba wake ukiwa unaelekea ukingoni, winga wa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Shiza Kichuya, amesema bado hajafikia uamuzi wa kusaini mkataba mpya na klabu hiyo kwa sababu ya kuangalia maslahi kwanza.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, ilimsajili Kichuya Julai mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar na kumpa mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza na Nipashe jana, Kichuya, alisema bado yeye na meneja wake hawajafikia uamuzi wa kusaini klabu yoyote mpaka sasa kwa sababu wanataka kuona mkataba mpya unakuwa na maslahi bora kuliko alichokuwa anapata sasa.

Kichuya alisema yeye atakuwa tayari kusaini mkataba ambao utamridhisha bila kujali klabu itakayomvutia iwe ya ndani au nje ya Tanzania.

"Bado sijafanya uamuzi wowote kuhusu kusaini mkataba mpya, nitamsikiliza meneja wangu kile ambacho ataniamulia," alisema kwa kifupi nyota huyo anayevaa jezi namba 25 mgongoni.

Hata hivyo, Kichuya hakuwa tayari kueleza kama anajiona tayari ameiva na anafaa kwenda kupambana kucheza soka la kulipwa kama ilivyo ndoto ya wachezaji wengi wa Tanzania baada ya kung'ara kwenye ligi ya nyumbani.

"Siwezi kusema lolote juu ya ofa za nje, akili yangu ni kuendelea kupambana na kusubiri kile atakachoniamulia meneja wangu," alimaliza Kichuya.

Moja ya maslahi ambayo Kichuya anataka yaboreshwe ni mshahara.

"Anafanya kazi kubwa sana, ni lazima Simba imuangalie kwa jicho linalostahili, endapo watamboreshea maslahi yake, nina hakika atasaini mkataba mpya bila shaka na akipata "dili" la nje atakwenda," kilisema chanzo chetu.

Taarifa kutoka Simba zimeeleza kuwa zipo klabu mbili za Misri zinazomhitaji Kichuya na zinasubiri akikataa kusaini tena Msimbazi zimnase kirahisi akiwa mchezaji huru.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad