Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizosambaa mitandaoni jana, Ndiku alifariki dunia kwa ugonjwa wa moyo saa chache mara baada ya kuhudhuria mazoezi ya timu yake ya Rayon Sports.
Ofisa Habari wa Rayon, Gakwaya Olivier alisema Ndiku ambaye alikuwa kocha wao msaidizi amefariki kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni ugonjwa wa moyo.
Staa wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ akifanya yake na Dogo janja.
“Alisikia maumivu makali kifuani, akaomba soda ya baridi wakamletea na alipomaliza kunywa tu kidogo, akatapika na akaishiwa pumzi,” alisema Olivier.
NIYONZIMA ANENA
Akizungumza na Amani, mchezaji wa Simba ambaye ni rafiki wa karibu na marehemu Ndiku, Haruna Niyonzima alisema rafiki yake huyo alilalamikia maumivu ya kifua mara baada kumaliza mazoezi kwisha akarudi nyumbani kupumzika lakini akatafuta daktari bila mafanikio ndipo akapelekwa hospitali ambapo mauti yalimpata ambapo uchunguzi wa awali ulionesha kuwa alikuwa na tatizo la moyo.
“Nimepokea kwa masikitiko sana kifo cha Ndikumana, nimezungumza na watu wa kule nyumbani (Rwanda), wamesema alishiriki vizuri mazoezi, mara baada ya mazoezi kumalizika alilalamikia maumivu ya kifua, akarudi nyumbani.
“Baada ya kufika nyumbani maumivu yaliongezeka, wakamtafutia daktari wa haraka ikashindikana ndipo wakalazimika kumkimbiza hospitali lakini bahati mbaya akafariki dunia alipofika hospitali ambapo baadaye iligudulika alikuwa na tatizo la moyo,” alisema Niyonzima.
Irene Uwoya akiwa ma Hamad Ndikumana ‘Ndiku’ siku ya ndoa yao.
WADAU SASA
Aidha, watu mbalimbali walipozungumza na Amani jana mara baada ya kupata taarifa za msiba, walikuwa na mawazo tofauti kuhusiana na kifo hicho cha ghafla huku wakikihusisha na ndoa ya Uwoya na Mbongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’.
“Jamani kwa kweli tuna shaka sana kuhusu kifo hiki, kwa muda mrefu Ndiku alikuwa mtu wa mawazo sana kuhusu mustakabali wa ndoa yake sasa ukijumlisha na hili tukio la juzi la Uwoya na Dogo Janja, huenda kikawa ndio kimemsababishia kifo,” alisikika Juma Sekio, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Sinza.
MWINGINE ANENA
Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Deo, alisema amekuwa akifuatilia posti za Ndiku kwa muda mrefu na kugundua kwamba anasumbuliwa sana na kitendo cha Uwoya kung’ang’ania talaka ili aolewe na mtu mwingine.
“Ndiku alikuwa hataki kumpoteza Uwoya. Alikuwa anaumia moyoni kwa muda mrefu. Alikuwa wakati mwingine anajifanya kwamba haumii kwa kuweka posti zake mitandaoni lakini ukweli ni kwamba alikuwa anateseka sana na penzi la Uwoya,” alisema mdau huyo.
DAKTARI AFUNGUKA
Akizungumzia kilichomuua, Dokta Leopard Mwinuka wa jijini Dar, alisema kuna uwezekano mkubwa sababu iliyosababisha kifo cha Ndiku ikawa ni msongo wa mawazo (stress) ambao umemsababishia presha.
Alisema kwa kawaida, mwili wa binadamu unapopata presha, kuna uwezekano mkubwa ukapata mshtuko wa moyo (heart attack) ambao unasababisha kifo cha ghafla.
Hamad Ndikumana ‘Ndiku’ enzi za uhai wake.
“Mshituko wa moyo hutokea wakati mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo. Iwapo mzunguko huo wa damu hautoendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo kusababisha kifo.
“Mpaka kufikia hatua mtu anapata mshtuko wa moyo, kuna vitu vinaweza kuwa vimetangulia. Kama ambavyo inaaminika Ndiku alikuwa na mawazo sana, ni dhahiri kabisa atakuwa amefariki dunia kwa mshtuko wa moyo,” alisema Dk. Mwinuka.
Akizungumza jana msibani nyumbani kwa Uwoya, Sinza- Mori, mama wa mzazi wa mrembo huyo, Naima Uwoya, alionesha kuguswa na msiba huo kutokana na jinsi alivyohangaika Ndikumana arudiane na mwanaye.
“Nimeshakwenda mpaka Israel kwa ajili ya kufanya maombi kurudisha ndoa yao, inaniuma sana jamani,” alizungumza huku akilia mama Uwoya.
Kwa upande wake Uwoya, hakuweza kuzungumza chochote zaidi ya muda mwingi kuonekana akilia kwa uchungu.
TUJIKUMBUSHE
Uwoya na Ndikumana walifunga ndoa Julai 11, 2009 ambapo waliishi kwenye ndoa kwa miaka kadhaa na kufanikiwa kupata mtoto mmoja aitwaye Krish kisha baadaye wakamwagana na kila mmoja akawa anaishi kivyake.
Kabla mauti hayajamkuta, Ndikumana alikaririwa akisema kuwa ameruhusu Uwoya aolewe na kwamba ameshatuma mtu nchini kwa ajili ya kushughulikia suala la kuivunja ndoa hiyo.
Hivi karibuni, Uwoya alidaiwa kufunga ndoa na Dogo Janja ambapo hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa si ndo bali picha zilizosambaa zilikuwa ni za tamthiliya ambayo inatarajiwa kuonekana hivi karibuni.
Chanzo: Global Publishers