Aliyekuwa waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Lazaro Nyalandu amefunguka na kudai kuwa Waziri wa sasa wizara hiyo Dkt. Hamisi Kigwangalla anatumika vibaya katika kumchafua na kueneza uzushi juu ya utumishi wake.
Nyalandu amefunguka hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook na kusema kwamba anasikitika kuona waziri huyo ametumia muda wake ndani ya bunge kumchafua, kumdhihaki pamoja na kusema uongo dhidi yake ikiwa anatambua kwamba ni njama za makusudi zilizopangwa kumchafua baada ya kuhama ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha Mh. Nyalandu amefunguka kwamba kinachofanywa juu yake ni hatua ambayo imepangwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi yeyote wa CCM atakayethubutu ama kudiriki tena kukihama Chama Cha Mapinduzi CCM katika Serikali ya awamu ya tano.
Nyalandu ameongeza kwamba Waziri "Kigwangalla anatumika vibaya, kwa u za uongo na uzushi aliuanza dhidi yangu mara tu alipoteuliwa, kwa kuanza kutoa kauli za kejeli dhidi ya utumishi wangu uliotukuka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wenye rekodi thabiti" - Nyalandu.
Ameongeza "Propaganda za Kigwangalla ameamua zimuhusu Waziri moja tu wa Maliasili, Lazaro Nyalandu, jambo linalothibitisha njama na Progaganda za kuzimisha moto na nguvu ya umma kupitia upinzani, hasa baada ya kitendo changu cha kukihama CCM".
Kati ya habari ambazo Mh. Nyalandu amedai kuwa ni za uzushi ni pamoja na Dkt Kigwangalla kusema bungeni kwamba kiongozi huyo alikuwa akitumia helikopta kugombea urais 2015 kitu ambacho Nyalandu amekipinga na kufafanua.
"Mwaka 2015 nilitumia Helicopter kwa siku tatu za kumalizia Kampeni, na nilikodi helikopta hiyo kwa Sh milioni tano kwa siku (Jumla, milioni 15). Pia ingependeza kama hamaki za Kigwangalla zingemkumbusha kuwa Waziri Nyalandu akiwa Wizarani alipatia Serikali Helikopta mpya Moja, alileta ndege kwa matumizi ya kupambana na Ujangili. Alishawishi benki ya dunia, Ujerumani na USA kuleta mamilioni ya dola za kmarekani kusaidia mapambano hayo, na kwamba alifanikiwa sana kutokomeza ujangili nchini. Rais Kikwete alikiri hili wakati wa kuzindua Tangazo la Tanzania (Tanzania, the soul of Africa)," Nyalandu.