Mahakama Kuu ya Tanzania leo Novemba 13, 2017 inatarajia kutoa hukumu katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili muigizaji wa filamu Tanzania Elizabeth Michael maarufu Lulu.
Kesi hiyo iliendelea mara ya mwisho Oktoba 26 mwaka huu chini ya Jaji Sam Rumanyika, ambapo baada ya kufunga kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka, na utetezi kwa upande wa mtuhumiwa alitangaza kuwa hukumu ya kesi hiyo itatolewa mahakamani hapo Novemba 13.
Katika kesi ya msingi, Lulu anatuhumiwa kumuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu (PC) aliyekuwa mwigizaji mwenzake wa filamu, Steven Kanumba Aprili 7, 2012 nyumbani kwa marehemu Sinza Vatcan, jijini Dar es Salaam.
Wazee wa Baraza ambao hutoa ushauri kwa hakimu anayeendesha kesi za mauaji walisema kuwa, Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia.
Hukumu hii imevuta hisia za watu wengi hasa waigizaji na wapenzi wa tasnia ya filamu nchini huku wengi wakimuonea huruma Lulu na kuomba ashinde au kupewa adhabu iliyo nyepesi kwa sababu hukumu itakayosomwa leo itafungua ukurasa mpya katika maisha yake.
Kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 198 cha kanuni za adhabu, mshtakiwa anayepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia adhabu ya juu kabisa huwa ni kifungo cha maisha jela.
Aidha, adhabu ya chini huwa ni kuachiwa huru kwa masharti maalumu au kifungo cha nje, ambapo ama mshtakiwa huonywa asifanye kosa jingine ndani ya muda maalumu unaopangwa na mahakama au anaweza kuamuriwa kufanya shughuli za jamii.
Leo Ndio Leo....Hatma ya Lulu kubaki uraiani au Gerezani Kujulikana
0
November 13, 2017
Tags