Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesitisha utoaji wa huduma za usafiri kwa kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro Express Limited baada ya kushindwa kulipa kodi ya Sh500 milioni.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameliambia gazeti la Mwananchi leo kuwa, wamefikia uamuzi huo baada ya majadiliano ya muda mrefu na kampuni hiyo kutokuzaa matunda.
Kayombo amesema biashara kwa kipindi cha hivi karibuni haikuwa nzuri kwani mabasi yake 26 yalipungua hadi kufikia 12 lakini si kigezo cha kutokulipwa kwa kodi ya Serikali.
“Ni kweli Kilimanjaro Express inadaiwa Sh500 milioni jambo ambalo lilitufanya sisi kusimamisha shughuli tangu Jumatatu (ya Novemba 13) hadi hapo atakapolipa kodi anayodaiwa,” amesema Kayombo
Kwa upande wake, mmiliki wa kampuni hiyo, Roland Sawaya amesema wamezuia mabasi yake ambayo yalikuwa yameegeshwa katika ghala mjini Moshi mkoani Kilimanjaro huku akieleza kuwa ni kweli anadaiwa lakini amekuwa akilipa deni hilo kwa awamu.
Amesema hivi karubuni alilipa Sh50 milioni na mwezi huu walitaka kulipa Sh35 milioni lakini TRA walikataa na kuwataka kulipa kiasi chote kilichobaki cha Sh500 milioni huku akieleza kwamba mazungumzo yanayoendelea ana imani yatafikia mwafaka na kurejea kutoa huduma.
Chanzo: Mwananchi