Mabasi ya Mwendokasi Kupanua Wigo Sasa Hadi Sinza, Masaki

Mabasi ya Mwendokasi Kupanua Wigo Sasa Hadi Sinza, Masaki
WAKALA wa  Mabasi Yaendayo Haraka (DART) unatarajia kupanua wigo wa usafiri huo kwa kuongeza ruti za Sinza, masaki na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sambamba na ruti hizo, DART pia inatrajia kuongeza mabasi katika mfumo wake kutoka 140 yaliyopo sasa hadi mabasi 305 pindi awamu ya kwanza ya mfumo huo itakapokamilika.

Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kupokea wageni sita kutoka serikali ya Rwanda ambao wako nchini kwa ziara ya siku tano ya kujifunza mradi huo unavyofanya kazi nchini.

“Tunatarajia kuwa hatua ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, itaongeza idadi ya watumiaji wa mabasi ya mfumo huo kutoka 200,000 kwa siku   kufikia watumiaji 400,000 hadi 500,000 kwa siku,” alisema.

Mhandisi Lwakatare alisema mradi huo utaongeza njia  kutoka mbili zilizopo sasa hadi njia  tisa, hivyo kupanua huduma ya usafiri katika maeneo mbalimbali yaliyomo ndani ya mfumo wa DART katika awamu ya kwanza ya mradi.

“Awamu ikikamilika tutakuwa na njia tisa, kuna nyingine zitakuwa zinaenda Masaki, Sinza, Chuo Kikuu na maeneo mengine ambayo yako jirani,” alisema.

Kuhusu athari zilizotokana na mvua zilizonyesha Oktoba 26,  mwaka huu, Mhandisi Lwakatare alisema mfumo wa mabasi uliathiriwa na mvua hizo na mabasi 40  yaliharibika na kati ya hayo 20  yaliharibika zaidi.

Hata hivyo, alisema mabasi hayo  yameshatengenezwa na yameanza kutoa huduma na kwamba wamejipana kuhakikisha mitaro yote inayozunguka karakana ya Jangwani inasafishwa ili kuepuka eneo hilo kukumbwa tena na mafuriko.

“Tumefarijika kupokea ugeni kutoka serikali ya Rwanda kuja kutembelea mradi kwa lengo la kujifunza hatua tuliyofikia ukizingatia kuwa jiji la Kigali nalo lina mpango wa kuwa na mfumo kama huu,” alisema.

Timu hiyo inaongozwa na Rwagatore Etienne kutoka Mamlaka ya Jiji la Kigali akiwa na wataalamu washauri ambao ndio waliopewa kazi ya usanifu wa jiji la Kigali kuwa na mfumo wake wa mabasi yaendayo haraka.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad