MARAIS John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda waliweka historia jana baada ya kuzindua kituo cha pamoja cha forodha kitakachochochea ukuaji wa biashara kwa nchi zote mbili.
Kituo hicho cha aina yake, kipo katika mpaka wa Tanzania na Uganda, eneo la Mtukula.
Magufuli (maarufu JPM), ambaye yuko nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, alisema wakati wa ufunguzi wa kituo hicho na mwenyeji wake, Museveni, kuwa wafanyabiashara waliokuwa wakitumia muda mrefu kutoa mizigo katika eneo hilo sasa wataondokana na adha hiyo.
Alisema kumekuwa na ukwamishaji wa maendeleo baina ya viongozi na wafanyabiashara wanaopeleka na kuingiza bidhaa ndani ya nchi hizo kwa kufanya ukaguzi wa muda mrefu unaomfanya mtu kutumia zaidi ya dakika 20.
Rais Magufuli alisema kituo cha Mtukula kilikuwapo tangu mwaka 2011 na kuanza kufanya kazi mwaka 2015, huku kikitoa huduma kwa muda mrefu ili kukamilisha utaratibu.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kituo hicho kimegharimu Sh. bilioni 7.16 hadi kukamilika kupitia fedha iliyotolewa na Trademark East Afrika kupitia ufadhili wa Canada na Uingereza.
Naye Rais Museveni alisema katika kupanua sekta ya uchumi na maendeleo, shughuli za kilimo, ufugaji, viwanda ni nguzo katika kutoa ajira kwa wananchi wa Uganda na Tanzania.
Katika ziara hiyo ambayo Rais Magufuli ameongozana na mke wake, Mama Janeth Magufuli, yeye pamoja na Museveni walifungua walifungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post - OSBP) kilichojengwa kwa lengo la kurahisisha taratibu za kiforodha, uhamiaji na kuharakisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Sambamba na kufungua kituo hicho, marais hao jana waliweka jiwe la msingi katika mradi wa bomba la mafuta ghafi la kuanzia Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Sherehe hizo zilifanyika katika kijiji cha Luzinga, kilichoko katika mkoa wa Rakai nchini Uganda.