MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo amewatembelea wagonjwa 21 kati ya 35 waliotakiwa kupewa miguu ya bandia katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Msasani jijini Dar es Salaam na amewaomba wadau kuendelea kusaidia.
Makonda amewatembelea wagonjwa hao Ijumaa ya Novemba 17, mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa kampeni yake aliyoianzisha Agosti 15 hadi 18, mwaka huu wakati Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ilipokuwa imeandaa kliniki ya huduma tengamao ambayo ilihudhuriwa na takribani watu 650 waliokuwa na mahitaji mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo, amewaomba wadau na mashirika mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wagonjwa wenye ulemavu wa viungo hasa miguu ili kuwawezesha kutembea hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Katika kipindi cha kampeni hiyo, CCBRT kwa kushirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na Taasisi ya MoveAbility walikubali kutoa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu wa viungo 21 walioelekezwa kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu na kupewa miguu bandia.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alipotembelea wagonjwa hao, Mkuu wa Idara ya Utengamao CCBRT, Ruth Mlay alisema kuwa Idara ya Utengamao inao uzoefu mkubwa wa kuzalisha na kutengeneza viungo saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa viungo saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa viungo hasa kwa waliopatwa na kiharusi, polio na matatizo ya kuzaliwa nayo.
Wakati huohuo, kampuni ya usanifu wa majengo ya Spectrum Design imechangia kiasi cha milioni kumi kwa ajili ya kampeni hiyo ya kuwawezesha walemavu wa miguu kununua miguu bandia.