Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa na Makamu wa Rais Samia Suluhu ni miongoni mwa viongozi waliofika nchini Kenya kuiwakilisha Tanzania kwenye sherehe za kuapishwa rais wa nchi hiyo.
Kiongozi mwingine wa Tanzania ambaye amehudhuria sherehe hizo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki Dk Suzan Kolimba
Sherehe za kuapishwa Uhuru Kenyatta zinafanyika leo mjini Nairobi huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakiwa wanatarajiwa kushuhudia.
Taifa la Kenya leo linatekeleza shughuli muhimu ya kikatiba ya kumuapishwa kiongozi wa taifa hilo kufuatia ushindi wake wa marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26 uliosusiwa na upinzani.
Uhuru Kenyatta leo anaapishwa rasmi kuwa rais wa nchi hiyo kwa muhula wa pili baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu.
Uchaguzi uliofanyika Agosti ulifutwa na mahakama kutokana na kile kilichotajwa kuwa uchaguzi usio huru na haki.
Marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26 ulimpatia Kenyatta asilimia 98 ya kura huku waliojitokeza kushiriki katika shughuli hiyo wakiwa na asilimia 39.