Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Pombe Magufuli amewaonya wanachama wapya ambao wamehamia ndani ya chama hicho leo kwenye mkutano mkuu wa NEC unaoendelea Ikulu jijini Dar es salaam.
Wanachama hao ambao wamehamia na kutangazwa leo ni Mwanasheria Alberto Msando aliyekuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo, Mbunge wa zamani wa Nyamagana Laurent Masha aliyekuwa mwanachama wa Chadema pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema taifa Patrobas Katambi.
Wengine ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye naye alikuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo pamoja na Sophia Simba ambaye ameomba kurejeshewa uanachama baada ya kufukuzwa kwa muda.
Akiongea baada ya kuwapokea wanachama hao Rais Magufuli amesema, “Nawaomba msije mkabadilika tena, mmekuja huku na wanachama wamewakubali msirudi tena kule, hiki ni chama cha wote hata watoto watazaliwa watakikuta na watajiunga kwasababu kina misingi imara, kwahiyo msije huku kujaribu”.
Rais Magufuli amemaliza kwa kuwapa ruhusa ya kugombea nyadhifa mbalinmbali ndani ya chama na kwenye maeneo yao. “Nyie sasa mmepitishwa na mkutano mkuu wa NEC hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kuwapinga na kama kuna nafasi ya kugombea huko nendeni mkagombee ili mje mshiriki kuijenga nchi na Chama”.