Maswali yaibuka Kuhusu Taasisi ya Mikopo
0
November 12, 2017
Siku moja baada ya Serikali kuikana taasisi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi, maswali yameibuka yakihusisha uhalali wake kisheria, chanzo chake cha fedha na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi.
Akijibu swali la mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi kuhusu uhalali wa taasisi hiyo bungeni mjini Dodoma juzi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema siyo wizara yake wala Serikali inayoitambua taasisi hiyo ya Tanzania Social Support Foundation (TSSF).
Hata hivyo, Mkurugenzi wa TSSF, Donati Salla ameeleza kusikitishwa na kauli ya Waziri Ndalichako akisema haina nia njema ya kusaidia wanafunzi wanaotoka kwenye familia maskini.
Salla alisema tamko la waziri limetolewa wakati maofisa wa wizara hiyo wakiitembelea ofisi yao kuthibitisha nyaraka za uhalali wake.
Alisema maofisa wa wizara walikagua cheti cha usajili wa shirika hilo, katiba, andiko la mradi, mkataba wa TSSF na mfadhili ambaye ndiye chanzo cha fedha zinazotolewa kwa wanufaika na nyaraka zinazoshuhudia uwapo wa shirika hilo tangu mwaka 2011.
Salla alisema maofisa hao waliagiza nyaraka hizo zitolewe nakala na ziwasilishwe kwa katibu mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Licha ya mkurugenzi wa rasilimali watu wa wizara hiyo, Moshi Kabengwe kuieleza Mwananchi kuwa alitembelea ofisi za TSSF, hakuzungumzia uhalali wa nyaraka hizo bali alisisitiza taasisi hiyo inapaswa kupeleka nyaraka wizarani ili kuhakikiwa.
“Ni kweli tulitembelea, lakini tuliwaambia walete hizo nyaraka wizarani, siwezi kuzungumzia sana suala hilo,” alisema.
Akizungumza katika ofisi za Mwananchi Tabata Relini jijini Dar es Salaam akiwa na nyaraka hizo, Salla alisema wamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika yasiyo ya kiserikali, Sura ya 56, ya Sheria za Jamhuri ya Muungano, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.
Msajili wa mashirika yasiyo ya Serikali, Marcel Katemba alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko nje ya Dar es Salaam.
Uchunguzi wa gazeti hili kwenye tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, haukuonyesha jina la Tanzania Social Support Foundation.
Kuhusu hilo, Salla alisema walitumia jina la Doli Foundation kabla ya kubadilisha kuwa Tanzania Social Support Foundation.
“Kama hawajabadilisha jina hilo, litakuwa ni tatizo la tovuti yao,” alisema Salla.
Kuhusu Waziri Ndalichako kutokuwa na taarifa ya mkutano wa TSSF na taasisi za elimu ya juu Novemba 30, alisema wamepanga hivyo na walitarajia kumwalika.
Alipoulizwa kuhusu wanufaika wa mikopo hiyo, Salla alisema wameshapokea maombi 500 na tayari kuna wanufaika 198.
Hata hivyo, alisema wanafunzi hao bado hawajaingiziwa fedha zao hadi Desemba 20 akidai ni kutokana na mfadhili kutaka orodha ya walioomba mikopo.
Alilitaja shirika la The Panelope Cagney la Marekani kuwa ndilo linalotoa fedha za mikopo hiyo.
Hata hivyo, katika tovuti ya shirika hilo hakuna jina la TSSF katika orodha ya wanaofadhiliwa.
Mwananchi:
Tags