Mawaziri wa Zamani Wanavyogeuka 'Bubu'

Kila wakati Rais anapofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, kuna uwezekano wa kuingiza sura mpya, lakini pia kuacha baadhi.

Katika hali hiyo, idadi ya wabunge waliowahi kuwa mawaziri inazidi kuongezeka ndani ya Bunge, ambalo ni chombo cha kuisimamia Serikali, kuiwajibisha na kutunga sheria.

Mabadiliko yaliyofanywa na Rais John Magufuli hivi karibuni, yameongeza idadi ya mawaziri wanaorudi katika viti vya kawaida, na kumrudisha mmoja, George Mkuchika katika Baraza la Mawaziri.

Ndani ya muhimili huo wa nchi, sasa kuna takriban wabunge 30 waliopata kuwa mawaziri na manaibu katika tawala zilizopita zilizokuwa chini ya Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na sasa wa Rais John Magufuli.

Wakiwa ndani au nje ya Bunge, wamekuwa hawaonekani kuwa wakosoaji katika mijadala ya Bunge, ingawa wanaweza kutoa maoni yao kwa maandishi bila ya kuzungumza bungeni.

Kati yao ni wachache ambao wameonekana kusimama na kuikosoa Serikali, wakiongozwa na Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Hawa Ghasia, ambaye alikuwa Waziri wa Tamisemi hadi Novemba 2015.

Baadhi wanapoamua kukomaa huelekeza vita yao kwa mawaziri binafsi, kuonyesha kuwa ndio wanaoishauri vibaya Serikali.

Idadi hiyo ya wabunge, waliokula kiapo kutotoa siri za Serikali, inaongeza nguvu katika hoja ya wananchi katika mchakato wa kuandika Katiba mpya kuwa mawaziri wasitokane na Bunge.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema wabunge hao wanashindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yao ya kibunge kutokana na kuwahi kuwa ndani ya Serikali.

Alisema baadhi ya matatizo kama mikataba mibovu, sheria zisizojali rasilimali za nchi zimepitishwa na mawaziri na manaibu ambao walikuwapo katika baraza la mawaziri, hivyo kukosoa ni sawa na kujivua nguo.

“Unajua unaweza kukuta, kipindi akiwa ndani ya Serikali kuna makosa aliyafanya, hivyo anashindwa kuwa na uwezo wa kuikosoa kwa kuwa anajua kabisa akifanya hivyo yanaweza kumgeukia,” alisema. “Anayeweza ni yule aliyetekeleza majukumu yake vizuri.”

Miongoni mwa wabunge waliowahi kuwa mawaziri na kukosolewa sana kila mijadala inapoibuka na William Ngeleja, Andrew Chenge, Anna Tibaijuka, Ezekiel Maige na hivi sasa George Simbachawene.

Mbunda alisema ili kuwepo na Bunge imara, mawaziri wasitokane na Bunge.

Aliyewahi kuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga alisema “wanashindwa kuikosoa Serikali kwa kuwa wanaogopa wanaweza kutumia fursa hiyo kutoa siri za Baraza la Mawaziri hivyo inabidi watumie mbinu nyingine.

Dk Mahanga, ambaye amehamia Chadema, alisema si mawaziri au manaibu tu hata wabunge wengine wa CCM ambao hawajawahi kushika nyadhifa hizo, wamekuwa waoga kutokana na chama kuwabana. “Ndio maana mtu kama (aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro) Nyalandu ameamua kutoka huko kwani ukiikosoa Serikali, unachukuliwa hatua za kichama. Wapo wachache wanaofanya hivyo ila wengi wao ni waoga,” alisema

Baadhi ya wabunge hao ni Dk Mary Nagu (Hanang’), Chenge (Bariadi), Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga), Charles Kitwaanga (Misungwi), Mhandisi Gerson Lwenge (Wanging’ombe), George Simbachawene (Kibakwe),

Wengine waliobahatika kushika uwaziri au unaibu ni Nape Nnauye wa Mtama, Mhandisi Isack Kamwelwe (Katavi), Anastazia Wambura (viti maalum) na Ramo Makani (Tunduru Kaskazini).

Wengine ni Ezekiel Maige (Msalala), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Hawa Ghasia (Mtwara vijijini) na Shamsi Vuai Nahodha (Kijitoupele).

Pia wapo Dk Shukuru Kawabwa (Bagamoyo), Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Saada Mkuya (Welezo), Janeth Mbene (Ileje), William Ngeleja (Sengerema), Anne Kilango Malecela (kuteuliwa) na Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Mjini).

Wengine ni Margaret Sitta (Urambo), Dk Diodorus Kamala (Nkenge), Juma Nkamia (Chemba), Philipo Mulugo (Songwe), Dk Haji Mponda (Malinyi) na Mahmoud Mgimwa wa Mufindi Kaskazini.

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad