Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chadema Kata ya Sofi wilayani Malinyi, Riko Venance amewekwa chini ya ulinzi na polisi wakati akitembelea kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Mission.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alfonce Mbassa amesema bado hawajaambiwa kwa nini mgombea huyo anashikiliwa na polisi wakati sheria inamruhusu kutembelea vituo.
"Nimepewa taarifa kwamba mgombea wetu anashikiliwa na polisi na hivi ndio naelekea eneo la tukio, bado sijajua kwa nini amewekwa chini ya ulinzi, nitatoa taarifa baadaye," amesema Mbassa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro hajapatikana kuzungumzia tukio hilo, jitihada za kumtafuta bado zinaendelea.
Kata ya Sofi ina vijiji vitatu ambapo viwili vinaongozwa na Chadema na kimoja hakina uongozi kwani kilishindwa kufanya uchaguzi kutokana na migogoro ya mipaka.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 kata hiyo ilikuwa na wakazi 12,000 huku waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2014/15 wakiwa 8,700.
Mwananchi: