Mhasibu Aliyeondolewa kwa Vyeti Feki Adaiwa Kutumia Funguo Bandia Kuiba Fedha Hospitalini

Mhasibu Aliyeondolewa kwa Vyeti Feki Adaiwa Kutumia Funguo Bandia Kuiba Fedha Hospitalini
Mhasibu aliyeondolewa kazini kwa vyeti feki, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kuiba fedha katika Hospitali ya Mkoa wa Singida akitumia funguo bandia kuingia ofisi ya uhasibu aliyowahi kufanya kazi.

Edith Talasi (49), mkazi wa Minga mjini Singida anayetuhumiwa kuiba Sh873,000 imeelezwa alifanya kazi hospitalini hapo kwa muda na baadaye alirejeshwa katika kituo chake cha kazi ambacho ni Manispaa ya Singida.

Talasi anashikiliwa pamoja na Anthony Felix (51), ambaye ni mlinzi wa nyumba yake ya  kulala wageni iitwayo Nandau.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 22,2017 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea jana Jumanne Novemba 21,2017 saa 6:30 usiku katika hospitali ya mkoa.

Akielezea tukio hilo, amesema muuguzi wa zamu Shamir Omari (27) alipotoka mapokezi akielekea wodini alimwona mtu akiwa amesimama jirani na ofisi ya mhasibu ambaye baada ya kumsalimia aliondoka.

“Muuguzi aliamini mtu aliyemwona huenda  alikuwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa lakini aliporudi alimwona tena eneo lilelile hivyo alimshuku kuwa si mtu mzuri,” amesema Kamanda Magiligimba.

Amesema muuguzi alitoa taarifa kwa mlinzi wa zamu wa hospitali hiyo, Abubakari Jumanne ambaye alimweka chini ya ulinzi mtu huyo ambaye ni mtuhumiwa Felix.

Kamanda Magiligimba amesema mtu huyo alijitetea kuwa alifika hospitalini kuchoma sindano akionyesha dawa alizokuwa nazo.

“Wakati wanaendelea na mahojiano waliona makufuli mawili ya mlango wa nje wa chuma yapo chini na mlango ukiwa wazi. Mtuhumiwa alieleza bosi wake kwa wakati huo alikuwa ndani ya ofisi ya mhasibu amejifungia ndani,” amesema.

Amesema polisi walipatiwa taarifa na kufika eneo la tukio ambako walikutwa mlango ukiwa umefungwa kwa ndani.

Kamanda Magiligimba amesema mhasibu wa hospitali alipoamriwa afungue mlango kwa kutumia funguo zake, mtuhumiwa Edith akikutwa akiwa amejibanza kwenye kona ya mlango.

Amesema watumishi wa hospitali hiyo walimtambua kuwa aliwahi kufanya kazi hapo.

Alipohojiwa ameingiaje ndani, Kamanda Magiligimba amesema alionyesha funguo saba na zilipojaribiwa zilifungua milango yote ya ofisi ya mhasibu.

Amesema mbali ya wizi wa Sh873,000, imeelezwa Aprili,2017 wahasibu wa hospitali hiyo walibaini upotevu wa Sh1.8 milioni na Oktoba mwaka huu walibaini upotevu wa Sh3.6 milioni.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk David Mwasita amekiri kutokea upotevu wa fedha hizo na kwamba wahasibu walilipa kwa fedha zao za mishahara.

Dk Mwasita amesema wahasibu walilazimika kutoa fedha zao binafsi hivyo wasingeweza kutoa taarifa ya upotevu kwa kuwa milango na sefu ilikuwa imefungwa kama kawaida.

Kamanda Magiligimba amesema  wanaendelea kuwahoji watuhumiwa na baada ya mahojiano kukamilika watafikishwa mahakamani.
Chanzo: Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad