Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Joshua Nassari amemnadi mgombea udiwani wa Kata ya Ambureni, Dominick Mollel kwa kugawa CD anazodai zinaonyesha namna baadhi ya madiwani wa chama hicho wilayani Arumeru walivyoshawishiwa kupokea rushwa ili kujiuzulu Chadema na kujiunga na CCM.
Mhe. Nassari aliyekuwa ameambatana na mbunge wa Bunda, Esther Bulaya aligawa zaidi ya nakala 500 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Kwa Pole wilayani humo huku akiwataka wananchi kutowachagua wagombea wa CCM kwa madai baadhi yao wanatuhumiwa kupokea rushwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Nassari amesema pamoja na kuwasilisha ushahidi wake Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ameamua kugawa nakala hizo kuwafungua macho wananchi waelewe kwamba wagombea kutoka CCM hawafai.
Nassari amewambia wananchi waliofurika katika mkutano huo kwamba wagombea kutoka chama tawala hawastahili kuchaguliwa kwa kuwa baadhi yao walijiuzulu kwa kutuhumiwa kupokea rushwa. Pia alizungumzia kitendo cha baadhi ya wagombea wa CCM kutoa ahadi ya kuyakomboa baadhi ya mashamba yaliyotwaliwa na wawekezaji wilayani humo na kudai kwamba wakati wao wanatoa ahadi jukwaani wao wataingia shambani kudai haki.
“Wakati wao wanaahidi kushughulika na nyaraka sisi watatukuta shambani tunaendelea na kazi sawa.” amesema Mhe. Nassari.
Chanzo : Mwananchi