Msajili wa Vyama Atoa Onyo kwa Vyama vya Siasa

Msajili wa Vyama  Atoa Onyo kwa Vyama vya Siasa
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amevionya vyama vya siasa na kutaka vifanye kampeni kwa kufuata sheria, vikijiepusha na vitendo vya matusi na uchochezi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili hii Novemba 19,2017 na Jaji Mutungi amesema maneno ya uongo, matusi na uchochezi kwenye kampeni ni kinyume cha sheria.

Sina shaka na mwitikio wa ushiriki wa vyama vya siasa katika kampeni za Uchaguzi mdogo wa madiwani unaendelea nchini katika kata 43 zilizoanza Oktoba 26 na zinazotarajiwa kuhitimishwa Novemba 25 mwaka huu, hata hivyo, zimebainika kasoro ndogo ndogo ambazo si ishara nzuri kuelekea uchaguzi wa amani.

Siyo jambo lenye tija kuacha kasoro hizi ziote mizizi, tunastahili kukemea kasoro hizi kwa nguvu zote, hivyo naviasa vyama vya siasa na wagombea wote wanaoshiriki katika uchaguzi huu mdogo wa madiwani kujiepusha na yafuatavyo:-

a) Kuepuka kutumia maneno ya uongo na yenye kuudhi, matusi, uchochezi, kashfa, na mambo yanayofanana na hayo kwani ni kinyume na sheria na , badala yake vyama vinadi sera zao;

b) Kuepuka vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapiga kura.

c) Kutochukua hatua za kisheria mkononi na kutojihusisha na vitendo vya uchokozi mfano kuingilia mikutano ya kampeni ya chama kingine, kuchoma ama kuchana bendera/ mabango ya chama kingine ;

d) Kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa, mfano kununua wapiga kura au kuuza shahada ya mpiga kura;
e) Kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapiga kura.

Aidha ni vyema vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huu pia kuelewa kuwa, vina wajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na wagombea wao kuheshimu na kufuata Sheria zote zinazohusika. Hivyo, kila chama kitekeleze wajibu wake, ili uchaguzi huu ufanyike kwa amani na utulivu.

Pia ninawaomba sana Waandishi wa habari kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi zenu wakati huu wa kampeni na uchaguzi ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi.

Ifahamike kwa wadau wote kwamba, maafisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wapo katika kata zote 43 wakifanya uangalizi wa karibu kubaini ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za uchaguzi.

Lengo kuu ni kuhakiksha kuwa kunakuwepo uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi, hakuna chama chochote kinachoingilia mikutano ya chama kingine kwa kufanya vurugu, kuepusha matumizi makubwa ya fedha na kuweka uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali nyingine katika kampeni. Hivyo kila chama cha siasa ambacho kinashiriki katika uchaguzi kinapaswa kuwashawishi wananchi kwa sera zake na si vinginevyo.

Miongoni mwa majukumu ambayo yanatekelezwa na maafisa wa ofisi yangu kwa sasa katika kata hizo 43 ni pamoja na kutoa mafunzo elekezi kwa vyama vya siasa, wagombea wa Udiwani, viongozi wao na wananchi kwa ujumla juu ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi na matendo yaliyokatazwa wakati wa kampeni na uchaguzi na kutoa taarifa juu ya mwenendo wa kampeni. Naamini elimu hii itaendelea kuwaongezea Umma ufahamu wa dhamira nzuri ya Serikali katika kukuza demokrasia nchini.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ina jukumu la kisheria la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Kanuni zake katika chaguzi zote ikiwamo chaguzi ndogo za wabunge na madiwani.

Jaji Francis S.K. Mutungi

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA

19 Novemba, 2017
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad