Mbunge wa Mtama kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema kwamba haamini katika masuala ya kuhama chama cha siasa kwa sababu kila chama kina itikadi yake na kwamba, itikadi ni sawa na imani ambayo mtu hawezi kuhama kienyeji kama inavyodhaniwa.
Nape ambaye amewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo alisema endapo kwenye chama chake kutakuwa na mapungufu, atayashughulikia akiwa ndani, na sio kuhama chama.
“Chama cha siasa ni itikadi, itikadi ni imani. Siamini sana katika kubadili imani kienyeji. Nitashughulikia mapungufu nikiwa ndani sio nje!,” aliandika Nnauye.
Katika maneno, Nape aliambatanisha na picha yake akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye alitangaza kukihama chama hicho kutokana na kile alichodai kuwa kimepoteza mwelekeo na kwamba hakiwezi tena kuisimamia serikali kama ilivyokuwapo awali.
Nyalandu ambaye amekitumikia Chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa alisema kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyigine, CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Oktoba 30 Nyalandu alitangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kusema kuwa angependelea kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa kidemokrasia na uhuru wa mawazo.
Tangu alipotenguliwa Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amekuwa akihusishwa na tetesi za kukihama chama hicho, jambo ambalo amekuwa akikanusha mara kwa mara akiamini kwamba hahitaji kuto