Mwanafunzi Aliyefariki kwa Kupigwa Radi Afaulu la Saba

Mwanafunzi Aliyefariki kwa Kupigwa Radi Afaulu la Saba
Aliyekuwa mhitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyamanzugo, Charles Samson ambaye alifariki dunia kwa kupigwa na radi Oktoba 19, ni miongoni mwa wanafunzi 6, 500 waliofaulu mtihani wa darasa la saba katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.

Mwanafunzi huyo alipigwa na radi alipokuwa akijisomea na wenzake kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.

Jumla ya wanafunzi 8, 600 walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba katika Halmashauri ya Buchosa.

Ofisa Elimu wa Kata ya Nyanzenda, Leogratus Rutanywanilwa alisema kwamba Samson amefaulu kwa kupata alama A.

“Wenzake wawili aliokuwa akijisomea nao pia wamefaulu mtihani huo na wanasubiri kujiunga na elimu ya sekondari mwakani,” alisema Rutanywanilwa.

Ofisa elimu hiyo pia aliwataja wanafunzi walionusurika katika tukio hilo ambao wote wamefaulu kwa kupata alama B, kuwa ni pamoja na Claud Mussa aliyekuwa anasoma Shule ya Msingi Luchili na Lutema Shilaka wa Shule ya Msingi Nyamabano.

Wanafunzi hao watatu walipigwa na radi Oktoba 19, walipokuwa wakijisomea katika jengo la Kanisa la AGT katika Kijiji cha Luchili wilayani Sengerema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu kufaulu kwao, mmoja wa watoto hao, Mussa aliyenusurika alisema kwamba hadi sasa bado wana kumbukumbu ya mwenzao.

Mama mzazi wa marehemu, Maria Mashauri aliwasihi watoto walionusurika katika tukio hilo kusoma kwa bidii na kufaulu kama njia ya kumuenzi mwenzao aliyetangulia mbele ya haki.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad