Mzee Majuto Afunguka Kuwa Kuna Watu Wasiojulikana Wanataka Kumuua

Mzee Majuto Afunguka Kuwa Kuna Watu Wasiojulikana Wanataka Kumuua
TAKRIBAN siku 10 baada ya kudai kutapeliwa milioni 25 na kampuni moja ya filamu (jina linahifadhiwa) mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, staa wa filamu za vichekesho Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ amefunguka kuwa, kuna watu wasiojulikana wanaotala kumuua, Ijumaa Wikienda limedokezwa.

Chanzo makini kililieleza Ijumaa Wikienda kuwa, staa huyo tangu atoe malalamiko ya kutapeliwa fedha zake hizo kwa Waziri Mwakyembe, amekuwa akiishi kwa wasiwasi huku akihisi kwamba anaweza kuuawa na watu wasiojulikana  kwa kuwa tu amedai haki yake.

“Yaani Mzee Majuto hana amani kabisa, amekuwa akilalamika kwamba kuna watu wanataka kumuua kwa kuwa tu alidai haki yake na mpaka sasa hajapata hata shilingi moja yupo tu, anahofia kuendelea kudai tena baada ya kumweleza waziri siku zilizopita na alipoteza namba yake ya simu kwenye ndege hivyo ameamua kunyamaza tu sasa,” kilieleza chanzo kutoka Tanga anapoishi Mzee Majuto.

Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni ili kuujua ukweli ambapo lilimtafuta Mzee Majuto akiwa nyumbani kwake, Tanga ambapo alikiri kweli kwamba kwa sasa anaogopa kuendelea kudai kwani anatishiwa kunyongwa au kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

“Licha ya kumweleza Waziri Mwakyembe, lakini mpaka sasa sijalipwa chochote na ninaogopa kuendelea kudai kwani natishiwa kuuawa, si unajua siku hizi mtu ukidai haki yako unaweza kunyongwa au ukiwa barazani kwako ukashtukia unapigwa risasi na watu wasiojulikana.

“Nilikuwa na namba ya Waziri Mwakyembe, nilimpigia mara moja baada ya siku zile kuniahidi atalishughulikia suala langu, lakini aliniambia yupo kwenye kikao nimtafute wakati mwingine.

“Siku chache baadaye nikiwa ninasafiri kwenye ndege nilipoteza simu na namba
ikapotelea hukohuko hivyo imebidi sasa nitulie nimwachie tu Mungu atanilipia hizo fedha ninazodai maana naogopa kunyongwa jamani,” alisema Mzee Majuto.

AMKUMBUSHA WAZIRI
Hata hivyo, Mzee Majuto alimkumbusha Wazi Mwakyembe kuhusiana na suala hilo ili amsaidie kwani peke yake ameshindwa kuendelea kudai kwa kuwa ana hofu kwamba anaweza kufanyiwa kitu mbaya.

TUJIKUMBUSHE
Oktoba 27, mwaka huu, Waziri Mwakyembe alikutana na wasanii mbalimbali kujadili changamoto za kazi ya sanaa nchini na kusema katika vitu ambavyo atapambana navyo ni pamoja na watu wanaowadhulumu wasanii haki yao na kuwaibia kazi zao za sanaa.

Waziri Mwakyembe alisema: “Mzee Majuto akaniomba kitu kimoja na kuniambia anaumwa anahitaji pesa, lakini ameshafanya kazi na kampuni (akaitaja) na ameshatengeneza filamu zaidi ya 100 kwa mkataba wa kulipwa fedha ndogo tu, shilingi milioni 25, lakini huu ni mwaka wa pili hajalipwa hata senti tano na nilimuahidi kulishughulikia.”

Waziri Mwakyembe aliendelea kufafanua kuwa kwa sasa yupo tayari kutumia fedha zake mfukoni kuhakikisha Mzee Majuto anapata haki yake kwa kazi mbalimbali alizofanya na kampuni hiyo.

Source: Global Publisher


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad