July7, 2017 kupitia mtandao huu wa Bongo5 niliandika makala yenye kichwa ‘Rayvanny itanichukua muda kukuelewa’. Hii ilikuwa mara baada ya kushinda tuzo ya BET 2017 katika kipengele cha International Viewers Choice na kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kushinda tuzo hiyo.
Nilitoa hoja kadhaa za kuchelewa kumuelewa Rayvanny kama vile kushinda tuzo hiyo bila kufanya kolabo na msanii yeyote mkubwa kutoka nje na mwisho ni kushinda tuzo kubwa nje wakati Tanzania hajawahi kupata tuzo yoyote, hivyo nikatamatisha kwa kueleza Rayvanny amekuwa mwanaume kabla ya mvulana.
Ushindi wa Nandy AFRIMA 2017
Usiku wa kuamkia jana ndipo tuzo hizo za AFRIMA zilitolewa nchini Nigeria na msanii Nandy kushinda katika category ya Best Female Artist In Eastern Africa Award.
Katika category hiyo Nandy amefanikiwa kuwabwaga wasanii kama Chess Nthussi, Feza Kessy, Juliana Kanyomozi, Lady Jaydee, Vanessa Mdee, Victoria Kimani na Wayna Wondwossen. Ushindi wa Nandy AFRIMA hauna tofauti na ule wa Rayvanny BET kulingana na hoja ya mwisho kuitoa hapo awali.
Kwa maana ipi?, inafahamika na ipo wazi Tanzania kwa sasa hakuna tuzo zozote za muziki zinazotolewa baada ya Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) kusitishwa kutolewa. Kipindi alichoanza kusikika Nandy hakuweza kushiriki hivyo hana tuzo hiyo, hivyo ushindi huo ni kufika 10 bila kupita kenda.
Alikiba na Nandy
Hawa ndio washindi pekee kwa Tanzania kutoka AFRIMA kwa mwaka huu, Alikiba ameweza kushinda tuzo mbili katika category za Best Africa Collaboration na Best Artist or Group in Africa RnB and Soul.
Kwanini nasema ‘Itapendeza zaidi kumpongeza Nandy kuliko Alikiba AFRIMA 2017’, si kwa maana mbaya ila kwa kujaribu kulinganisha na kutofautisha mambo matatu yafuatayo;.
Mosi; Kama nilivyotangulia kueleza hii ni tuzo ya kwanza kwa Nandy ni wazi anastahili pongezi lakini kwa upande wa Alikiba licha kushinda tuzo mbili kwake ni kitu ambacho kimeshajitokeza mara kadhaa ameshashinda tuzo mbali mbali kubwa.
Kwa mwaka huu Alikiba amekabidhiwa tuzo ya MTV EMA aliyoshinda katika category ya Best African Act aliyoshinda mwaka jana ambayo alikabidhiwa kimakosa Wizkid, hivyo ushindi wa AFRIMA hauwezi kushtua mashabiki wake kama itavyokuwa kwa upande wa Nandy.
Pili; Wakati tuzo za KTMA zinatolewa kwa mara ya mwisho June 2015 Alikiba aliweza kujichotea tuzo tano, huu ulikuwa si ushindi wake wa kwanza katika tuzo hizo, hivyo hata alipoanza kushinda tuzo kubwa za nje alikuwa tayari ana msingi mzuri kwa hapa Bongo kitu ambacho ni tofauti kwa Nandy kama nilivyoeleza hapo awali.
Tatu na mwisho; Jitihada za kuipata tuzo yenyewe, ni wazi kuwa Nandy alikuwa na shauku kubwa ya kushinda tuzo hizi kuliko Alikiba kwa kuangalia haya mambo mawili. Kwanza, kuhudhuria, Nandy aliweza kwenda nchini Nigeria ukilinganisha na Alikiba ambaye hakuhudhuria kabisa kutokana na sababu zake binafsi.
Jambo la pili ni kuomba kura kutoka kwa mashabiki, nimetembelea ukurasa wa Instagram wa Nandy na kukuta namna alivyokuwa akihimiza mashabiki wake kumpigia kura.
Alifanya hivyo August 10, October 6 &13 na mara ya mwisho ilikuwa November 10 lakini Alikiba hakufanya hivyo hadi pale aliposhinda ndipo alipojitokeza katika mtandao huo na kuwashukuru mashabiki wake wote wa Tanzania na nje waliompigia kura hadi kupata ushindi huo. Naomba kuwasilisha.