Mlinzi wa kimataifa wa Tanzania anaecheza soka nchini Ujerumani kwenye klabu ya VfB Eppingen inayoshiriki Ligi Daraja la Tano, Emily Mugeta amesema anamshukuru Mungu baada ya hali yake kuendelea kutengemaa baada ya kufanyiwa upasuaji.
Mugeta alifanyiwa upasuaji wa bega lake baada ya kuumia vibaya wakati akiitumikia timu yake huku upasuaji huo ukiwa ni wa pili baada ya ule wa kwanza uliohusisha bega hilo hilo kufanikiwa licha ya kuhitajika kukaa nje ya uwanja msimu mzima.
Mugeta aliyepata kucheza kwenye klabu ya Simba aliiambia shaffihdauda.co.tz kuwa: “Ndiyo, nimefanyiwa upasuaji wa bega, maendeleo si mabaya,” alianza kueleza nyota huyo. “Niliumia wakati nikiitumikia timu yangu kwenye mechi, wameniambia nitakaa nje kwa miezi 10, yaani msimu mzima kwani niliumia vibaya sana.”
Licha ya kutarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima, matibabu ya nyota huyo yamegharamiwa na timu yake, VfB Eppingen lakini mwenyewe haachi kumshukuru Mungu kwa yote yaliyojitokeza kwani ndie mpangaji wa yote.
Emily Mugeta anaongeza idadi ya majeruhi wanaoiandama Tanzania baada ya nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbana Samatta kufanyiwa upasuaji huko Ubelgiji na nyota mwingine wa Tanzania, Farid Mussa kuripotiwa kuwa majeruhi pamoja na Thomas Ulimwengu.