Omog Aanika Wachezaji Watakaotemwa

Omog Aanika Wachezaji Watakaotemwa
KUSHUKA kiwango na kuwa majeruhi wa muda mrefu ni moja ya sababu ambazo Kocha wa Simba, Joseph Omog, amesema zitachangia kufanya uamuzi wa "kutema" baadhi ya wachezaji wake katika kipindi cha dirisha dogo la usajili wa wachezaji linaloendelea nchini.

Baadhi ya nyota wanaoonekana kukalia kuti kavu kwa kuzingatia sababu zilizotolewa na Omog ni pamoja na majeruhi Saidi Mohammed (kipa), Shomari Kapombe (beki) na straika Nicholas Gyan ambaye ameshindwa kuonyesha makali yake kama alivyokuwa kwao Ghana.

Omog aliliambia gazeti hili kuwa anatarajia kukutana na viongozi wa Simba mwishoni mwa wiki ili kuwasilisha mapendekezo yake ambayo yanalenga kuimarisha kikosi chake.

"Tutakuwa na kikao na viongozi wikendi hii, sisemi ni idara gani ninataka kuiimarisha, lakini kwanza nitaanza na wachezaji ambao hawajaonyesha viwango vizuri na wale majeruhi wa muda mrefu," alisema Omog.

Alisema kuwa mbali na kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubahatisha ya Matokeo Michezoni ya SportPesa, inatakiwa pia ifanye vizuri katika mashindano ya Kombe la FA na michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika watakayoshiriki kuanzia mapema Februari mwakani.

"Tunatakiwa tuwe imara kila idara, tunaelekea kwenye hatua ngumu zaidi, tunahitaji kuwa na wachezaji ambao wanauwezo na uzoefu wa kuisaidia timu," Omog aliongeza.

Dirisha dogo la usajili lililofunguliwa tangu Novemba 15 na litafungwa ifikapo Desemba 15, mwaka huu, siku chache kabla ya Yanga na Simba zitakazochuana kwenye mashindano ya CAF kutakiwa kupeleka majina ya nyota wake iliyowasajili.

Simba ambayo msimu huu imefanikiwa kuondoka na pointi sita Mbeya, inaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwakaribisha Lipuli FC katika mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex uliyopo Chamazi jijini Dar es Salaam.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad