Katika siku za mwishoni mwa utawala wake, kila kauli ya busara, yenye hoja au tata ilihusishwa na aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
Uzee wake, umri wa miaka 93, haukumfanya ageuzwe babu wa kumtania na kumjazia kila kauli ya mtu anayeonekana kuwa ni msomi, bali kutokana na kuamini kuwa Mugabe alikuwa ni msomi aliyesoma vizuri na mwenye uwezo wa kujenga hoja.
Kwa hiyo haikuwa ajabu kwa mchakato wa kumtaka ajiuzulu urais kwa hiari yake, kuchukua muda mrefu tofauti na ilivyotarajiwa baada ya jeshi kuingia kati ya kumuweka chini ya ulinzi nyumbani kwake.
Katika mapinduzi ya kawaida, jeshi lingetangaza kuishika nchi baada tu ya kufanikiwa kuishika ikulu, lakini katika dunia ya leo jeshi lisingepata ushirikiano na nchi jirani pamoja na jumuiya ya kimataifa. Hivyo ilihitajika ama Mugabe ajiuzulu mwenyewe, au mchakato wa kumuengua kikatiba uanze, jambo ambalo lingechukua muda mrefu na kukabiliana na vikwazo vya kisheria.
Njia rahisi, ilitakiwa iwe kumshawishi ajiuzulu, ili mambo mengine yaende kiulaini. Lakini nani angefanya kazi ya kuzungumza na kumshawishi mtu aliyejaa hoja? msomi aliyepikwa vizuri na mtu mwenye kushikilia anachokiamini?
Aliyebeba jukumu hilo kwa mafanikio alikuwa Padri Fidelis Mukonori, mtu ambaye enzi za ujana wake alikusanya ushahidi wa jinsi wananchi walivyofanyiwa ukatili wakati wa vita vya ndani na baadaye Mugabe, wakati huo akiongoza mapambano ya uhuru, kupata taarifa zake.
Baada ya miongo kadhaa, mwinjilisti huyo amefanya kazi nyingine ya kumshawishi Mugabe kung’atuka.
Alikuwa kinara wa mazungumzo ya kumshawishi Mugabe kuachia ngazi kwa sababu mwanasiasa huyo mkongwe na jeshi wote walimuamini.
“Mimi ni nafaka ngumu kuweza kuivunja,” alisema Mukonori alipofanya mahojiano na kituo cha televisheni cha CNN.
“Nilishawahi kufanya kazi hii.”
Mukonori alisema hayo katika mahojiano ya kwanza tangu kumalizika kwa amani kwa mabadiliko hayo ya uongozi nchini Zimbabwe baada ya Mugabe kuongoza taifa hilo kwa miaka 37.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu na nyumbani kwa Mugabe.
Mukonori, ambaye ana umri wa miaka 70 na Padri wa Kanisa la Katoliki wa Shirika la Jesuit, alikuwa akikutana na Mugabe kila siku, kwa mujibu wa CNN.
Kituo hicho kinamkariri Mukonori akisema kuwa mkakati wake ulikuwa si kubishana na Mugabe, bali kumsikiliza na kumshawishi Mugabe kwamba anaweza kuachia siasa kwa heshima.
“Ni mtu anayeweza majadiliano, anayefikiria, anatoa hoja kwa akili, anaweza kuweka hoja katika mtazamo wa kifalsafa,” Mukonori aliiambia CNN. “Ilikuwa ni suala la kumfanya Rais Mugabe aone kilichokuwa kinaitokea nchi kiuchumi na kisiasa kwa wakati huo na nini ilikuwa athari kutokana na jinsi wanajeshi walivyoingilia.”
Mugabe aliwekwa chini ya ulinzi wa wanajeshi nyumbani kwake wakati alipotangaza kujiuzulu Jumanne. Vikosi viliweka kambi Ikulu na katika jengo la bunge.
“Ukweli kwamba wanajeshi walikuwa wamechukua hatua hiyo-Mugabe hakukataa kwamba kulikuwa na tatizo, lakini alishangaa kwa nini ililazimika kufanyika hivyo,” alisema Mukonori katika mahojiano hayo.
Kwa kuwa jeshi lilisisitiza kuwa hatua hiyo haikuwa mapinduzi, bali njia ya kutatua mgawanyiko uliokuwa ndani ya chama tawala cha Zanu-PF, walilazimika ama kumshawishi Mugabe ajiuzulu au akabiliane na kuondolewa madarakani na Bunge ili kufuata katiba, jambo ambalo lingechukua muda mrefu.
Kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda, shinikizo lilikuwa kubwa kwa Mukonori na majenerali ili wafanye kitu kumaliza hali hiyo.
Mukonori anasema alimuhakikishia mara kwa mara Mugabe mchango wake katika uhuru wa Zimbabwe uliomfanya awe shujaa wa taifa. Ingawa anasakamwa na sehemu kubwa ya dunia, Mugabe bado anaheshimiwa na jeshi na uongozi wa chama tawala.
“Wakati wote majenerali walionyesha kumuheshimu wakati wa mazungumzo na hata walimpigia saluti,” alisema Mukonori. “Alijua angependa kuondoka kwa heshima.”
Pamoja na hilo, Mugabe alionekana kutaka kuendelea kukaa madarakani- hata kwa wiki chache.
Makubaliano yalifikiwa, lakini baada ya kuongoza kwa miaka 37 madarakani, Mugabe bado alitaka mabadiliko ya kumuachia madaraka Emmerson Mnangagwa yafanyike kwa utaratibu. Mnangagwa, ambaye alitimuliwa na Mugabe na kwenda kuishi nje kama mkimbizi, alikuwa akiwasiliana na majenerali wakati wote.
Wakati Mugabe alipohutubia taifa kwa kutumia televisheni ya serikali Jumapili iliyopita, karibu kila mtu alitegemea kuwa angejiuzulu. Lakini akiwa amezungukwa na majenerali, Mugabe alitumia hotuba yake ndefu kuzungukazunguka, lakini hakujiuzulu.
Mukonori alisema mchakato wa mazungumzo ulihitaji uvumilivu.
“Kumsikiliza mtu mwenye umri wa miaka 93 si sawa na kumsikiliza mtu mwenye umti wa miaka 23 au 17,” alisema.
Mwishoni, vilio vya Wazimbabwe waliokuwa wakiandamana, vilimshawishi aondoke, alisema Mukonori.
Wakati maelfu ya watu walipomiminika katika mitaa ya Harare kumtaka Mugabe aachie ngazi, padri huyo alitumia nafasi kukamilisha mchakato.
“(Maandamano) Yalimgusa,” alisema Mukonori. “Ilimgusa kwa maana kwamba aligundua kuwa walikuwa wakisema imetosha.”
Na alipojiuzulu, kulikuwa na shangwe kwa Wazimbabwe ndani na nje kushangilia mwisho wa utawala wake.
Mukonori alisema Mugabe alialikwa katika sherehe za kuapishwa kwa Mnangagwa, lakini alikataa, kutokana na mazingira hayo.
Padri huyo anasema anaendelea kuzungumza na Mugabe karibu kila siku. Alisema Mugabe ameahidi kutoa ushauri kwa rais mpya, licha ya Wazimbabwe wengi kutaka mwanzo mpya.
“Hajatoweka maishani, hajafa,” alisema Mukonori. “Lakini amepotea hadharani. Ubongo wake bado unafanya kazi na ni mzuri.”
Makala hii imetafsiriwa kutoka CNN