Rais John Magufuli amelaani uamuzi ulitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), ambayo imemuagiza mwendesha mashtaka wake kuanzisha uchunguzi dhidi ya mgogoro wa Burundi.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumamosi Novemba 11,2017 akiwa mjini Masaka nchini Uganda kabla ya kuagana na mwenyeji wake, Rais Yoweri Museveni baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku tatu.
Rais Magufuli katika taarifa ya Ikulu amesema majaji wa ICC wametoa uamuzi huo Novemba 9,2017 na kumtaka mwendesha mashtaka wa Mahakama hiyo kuchunguza vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu vilivyotokea Burundi tangu kuzuka kwa mvutano miaka miwili iliyopita.
Rais Magufuli amesema, “Hatua hii inarudisha nyuma jitihada zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyounda kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Rais Museveni na Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa.”
Amesema hali ya Burundi si mbaya kama inavyotangazwa kwa kuwa tayari wakimbizi wengi waliokuwa Tanzania wamerejea nchini humo, huku wengine wakiendelea kurejea.
Rais Magufuli amesema viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kutana Novemba 23,2017 kuendeleza mchakato wa utatuzi.
Akizungumzia hilo, Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema ICC inaingilia mambo ya jumuiya hiyo bila kuwahusisha viongozi wake jambo ambalo si sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi