Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ametenga siku moja kila mwezi kwa ajili ya ziara za kikazi katika wilaya zote saba mkoani hapa kusikiliza na kutatua kero za migogoro ya ardhi zinazowakabili wananchi.
Mongella alisema jana kuwa ziara hizo zitaanza Novemba 20, katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.
“Nitaanza na jiji la Mwanza ambalo ni kinara kwa kuwa idadi kubwa ya migogoro ya ardhi ambayo hutokana na utendaji mbovu wa baadhi ya maofisa wa idara ya ardhi,” alisema Mongella.
Alisema mwaka jana 2016, jiji hilo linaloundwa na Manispaa za Ilemela na Nyamagana lilikuwa na migogoro ya ardhi zaidi ya 1, 040 iliripotiwa.