Baada ya kuhukumiwa miaka tisa jela na mahakama ya Italia kwa kosa la ubakaji, mchezaji wa soka wa Brazil, Robinho amesema hakubaliani na hukumu hiyo kwani hakusika na tukio hilo kama ilivyoelezwa.
“Nimeshachukua hatua zote za kisheria kwaajili ya kujitetea, sikuhusika kwa namna yoyote kwenye tukio hilo kama ilivyodaiwa na tumekata rufaa kupiga hukumu hiyo”, amesema Robinho.
Mahakama ya Italia jijini Milan jana ilimhukumu Robinho pamoja na wanaume wengine watano raia wa Brazil kwenda jela miaka tisa kwa kosa la kumbaka binti mmoja raia wa Albania mwaka 2013. Hata hivyo mahakama imetoa muda kwa Robinho na wenzake kukata rufaa kabla ya kuanza kutumikia kifungo hicho.
Mahakama ilidai kuwa wakati binti huyo anabakwa mwaka 2013 alikuwa na umri wa miaka 22. Tukio hilo linadaiwa kufanyika kwenye club moja ya usiku jijini Milan ambapo Robinho na wenzake walimnunulia pombe nyingi binti huyo na baada ya kulewa ndio wakamfanyia vitendo hivyo.
Robinho mwenye umri wa miaka 33, alicheza AC Milan kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. Nyota huyo aliyeanza maisha ya soka kwenye klabu ya Santos ya Brazil pia amewahi kuzichezea timu za Real Madrid na Manchester City. Robinho kwasasa anachezea klabu ya Atletico Mineiro ya Brazil.