Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Augustine Mahiga ni miongoni mwa mawaziri wanaokutana kwa dharura mchana huu kujadili hali ya kisiasa nchini Zimbabwe ikiwa siku mbili baada ya jeshi kumweka kizuizini Rais Robert Mugabe.
Tanzania inashiriki kwenye mkutano huo kama mmoja ya wajumbe wa chombo kinachojulikana kama Troika.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), Rais Jacob Zuma ndiye aliyeitisha mkutano huo.
Baadaye amepanga kuzungumza na marais wenzake wa Sadc kwa ajili ya kuwapa taarifa juu ya kile kinachoendelea nchini Zimbabwe.
Mkutano huo umepangwa kufanyika Zimbabwe na utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, pia utahudhuriwa na mawaziri wengine kutoka Angola na Zambia.
Jana Jumatano, Rais Zuma alizungumza kwa njia ya simu na Rais Mugabe na kueleza kwamba kiongozi huyo alikuwa amezingirwa nyumbani kwake lakini alikuwa salama. Mugabe (93) ameitawala Zimbabwe tangu taifa hilo lilipopata uhuru 1980.
Wakati huohuo ,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amehimiza kuwepo utulivu nchini Zimbabwe na kuzitaka pande zote kujiepusha na matendo yanayoweza kulivuruga taifa hilo.
Amesema njia bora ya kupatikana kwa suluhu ya kisiasa ni ile inayozingatia majadiliano na mazungumzo ya amani na wala siyo vinginevyo.
Kupitia msemaji wake, Farhan Haq, Guterres amesema anafuatilia kwa karibu yale yote yanayoendelea nchini humo. Pia ameelezea matumaini yake kuhusu juhudi zilizoanza kuchuliwa na jumuiya ya Sadc kuhusu mzozo huo.
Kauli ya Guterres inatolewa huku hatma ya Rais Mugabe ikibakia kuwa kitendawili baada ya kuzuiliwa katika makazi yake.
Wakati huohuo, Umoja wa Afrika (AU) umesema kuwa hatua ya jeshi la Zimbabwe ya kuchukua madaraka na kumzuilia Rais Mugabe inaonekana kama mapinduzi wa kijeshi.
Mkuu wa kamisheni ya umoja huo, Alpha Conde amesema AU inataka kurejea mara moja hali ya kawaida.
Wakikosea pia mkutane
ReplyDelete