Serikali imewasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na imeweka vifungu vikali vya kukabiliana na biashara ya dawa za kuelevya nchini.
Katika mabadiliko hayo ya sheria maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya sasa wataruhusiwa kumiliki silaha na kutumia silaha za moto inapobidi.
Katika muswada huo, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Masuala ya Ukimwi imetaka wakati wa kutunga kanuni za sheria hiyo, Serikali iingize pombe aina ya viroba katika orodha ya dawa za kulevya.
Akiwasilisha muswada huo, waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenister Mhagama alisema mabadiliko hayo yataongeza ukali wa vita dhidi ya biashara hiyo.
Akizungumzia maofisa wa mamlaka kumiliki silaha, Mhagama alisema nguvu ya kifedha ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya inawafanya wamiliki silaha na kujiwekea kinga ya ulinzi.
“Hii inafanya mazingira ya kiutendaji kuwa hatarishi wakati wa ukamataji. Kwa sasa mamlaka inatumia polisi kwa ajili ya ulinzi wakati wa kufanya operesheni zake za ukamataji watuhumiwa,” alisema.
Mhagama alisema kuna wakati taarifa hupatikana usiku na kuhitaji utekelezaji wa haraka, hali ambayo hulazimu maofisa wa mamlaka kujitoa muhanga na kuhatarisha usalama wao au kuahirisha.
Chini ya mabadiliko hayo, mtu atakayemsafirisha mtu mwingine nje ya nchi kwa minajili ya kuwekwa rehani ili kufanikisha biashara ya dawa za kulevya, atahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mbali na hilo, sheria hiyo mpya imeongeza makosa yasiyostahili dhamana kuwa ni pamoja na kumiliki mitambo ya kutengeneza dawa za kulevya na kufadhili biashara hiyo ya dawa za kulevya.
Halikadhalika mtu atakayekamatwa kwa tuhuma za kuwaingiza watoto kwenye biashara na matumizi ya dawa za kulevya, hawataruhusiwa kupata dhamana watakapofikishwa mahakamani. Katika sheria hiyo mpya mtu atakayetiwa hatiani kwa makosa ya kujihusisha na biashara hiyo mali zake na za washirika wake ambazo alizipata miaka 10 kabla ya kutiwa hatiani zitataifishwa.
Mhagama alisema marekebisho hayo yameweka utaratibu mzuri wa kufanya makubaliano baina ya Tanzania na nchi za nje ya namna ya kusaidiana kutaifisha mali.
Alisema marekebisho hayo ya sheria yanampa uwezo kamishna jenerali wa mamlaka hiyo kushikilia akaunti za watuhumiwa benki ili kuimarisha na kuboresha uchunguzi.
Pia, marekebisho hayo yameweka kifungu kinachotambua kuwa itakuwa ni kosa kusafirisha isivyo halali kemikali zinazotumika katika kutengeneza dawa za kulevya.
Akitoa maoni na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Ukimwi, Dk Jasmine Bunga alisema inakubaliana na marekebisho hayo ya Serikali ili kupanua wigo wa vita hiyo.
Dk Bunga alisema wakati wa kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo, Serikali ione umuhimu wa kuongeza kwenye orodha viroba na dawa nyingine za binadamu kama za kulevya.
Alisema dawa hizo nyingine za binadamu zipo zinazoweza kutumiwa kama dawa za kulevya na hiyo itasaidia kudhibiti mbinu mpya za kuzalisha dawa mpya za kulevya hapa nchini.
Vilevile kamati hiyo iliitaka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya idhibiti taarifa na ripoti za uchunguzi kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuondoa mazingira ya ubambikiaji kesi.
Dk Bunga alipendekeza mamlaka za Tanzania Bara na Zanzibar kutafuta mbinu za kudhibiti mianya ya kupenyeza dawa za kulevya Zanzibar kwa kuwa sheria inahusu Tanzania Bara tu.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa wizara hiyo, Masoud Salim alitahadharisha kuwaruhusu maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kumiliki na kutumia silaha kuwa ni hatari zaidi.
“Kuruhusu maofisa wa chini ya mamlaka hii kutumia silaha bila kueleza utaratibu wa mafunzo maalumu yanayotambuliwa kwa mujibu wa sheria ni hatari zaidi,” alisema.
Salim alisema sheria hiyo inamruhusu ofisa wa mamlaka kufyatua risasi au kutumia silaha kwa mtu anayehisiwa kutumia au kuuza dawa za kulevya anapotaka kukimbia au kuleta hatari.
“Ikumbukwe kuwa mwenye mamlaka ya kumkamata raia yeyote anayehisiwa au aliyetenda kosa kinyume cha sheria ni askari aliyepewa mafunzo,” alisema na kuongeza:
“Kitendo cha kuwaruhusu maofisa hawa ambao hawajaelezwa kama wanayo mafunzo ya kukamata au utaalamu wa kushughulika na wahalifu kuwapa mamlaka makubwa ya silaha ni hatari.”
Kambi hiyo ilitaka sheria hiyo iwe ke msisitizo wa kuwabana na kutoa mafunzo yenye tija ili kutoruhusu mwanya wowote wenye nia ovu kwa ofisa ambaye atakosa weledi katika majukumu yake.