Kaimu Meneja uhusiano na Masoko wa Shirika la Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF), Salim Khalfan Kimaro, ameeleza kuwa ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara inayopita katika daraja hilo, fedha za makusanyo, pamoja na miundombinu, wapiga picha wote watapaswa kufuata utaratibu maalumu.
“Tumetoa taratibu maalum za kupiga picha baada ya kuzingatia hali halisi ya pale darajani ili kuwe na usalama wa wapiga picha wenyewe, lakini pia wapita njia pamoja na magari yanayokatisha pale na eneo letu la makusanyo kwa maana ya usalama wa fedha za makusanyo,” alisema Kaimu Meneja Kimaro.
Kaimu Meneja Kimaro alisema kuwa wapiga picha wote watapaswa kuomba kibali kwa Mkurugenzi Mkuu ambapo wataelekezwa kwa Afisa msimamizi wa mradi wa daraja la kigamboni ili wapewe maelekezo ya mahali salama na mahususi kwa kupigia picha.
Kimaro aliongeza kuwa kwa wale wanaopiga picha maalumu kama vile za harusi, video za kwaya na wasanii wa miziki mingine, watapaswa kulipia kiwango maalumu kilichowekwa ili waweze kupata huduma hiyo.
“Wale wanaopiga picha za matukio maalum watalipia kiwango fulani ambapo kwa saa moja ni 250,000 na kwa nusu saa ni 125,000,” alisema Kimaro.
Aidha kaimu Meneja kimaro alieleza kwamba wapiga picha wanaopiga picha moja moja ama ‘selfie’ hawatolipia lakini amewataka kuhakikisha kuwa wanachukua tahadhari ya usalama wao pamoja na watumiaji wengine wa barabara katika daraja hilo.