Ofisi ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) imesimamisha shughuli za Shirika la Tanzania Social Support Foundation (TSSF) kuanzia tarehe 14/11/2017 ili kupisha uchunguzi.
Taarifa ya ofisi hiyo imesema kuwa serikali inafanya uchunguzi juu ya tuhuma zinazolikabili shirika hilo za kutapeli watu mbalimbali nchini kwa kisingizio cha kuwapatia mikopo kwa ajili ya elimu ya juu kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Aidha serikali imeagiza kusimamishwa kwa shughuli zote za shirika hilo ikiwa ni pamoja na kufunga ofisi zote za shirika hadi uchunguzi utakapokamilika.
Viongozi wa shirika hilo wameagizwa kufika katika Ofisi ya msajili mara moja wakiwa na nyaraka halisi za usajili wa Shirika ambavyo ni Cheti na Katiba kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.