Vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara Simba SC wamelazimishwa sare ya 1-1 na klabu ya Lipuli FC kwenye mchezo wa raundi ya 11 uliomalizika jioni hii uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Simba walitangulia kwa bao la mapema lililofungwa na kiumgo Mwinyi Kazimoto dakika ya 15 kabla ya Lipuli FC inayofundishwa na nahodha wa zamani wa Simba Suleiman Matola kusawazisha kupitia kwa Asante Kwasi dakika ya 19.
Baada ya mchezo wa leo Simba imebaki kileleni ikiongoza kwa alama 23 alama moja zaidi ya Azam FC yenye alama 22 ikiwa na mchezo mmoja mkononi. Lipuli FC sasa imefanikiwa kutoa sare dhidi ya timu za Simba na Yanga kwenye uwanja wa Uhuru ambapo kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi ilitoka sare ya 1-1 na Yanga.
Raundi ya 11 ligi kuu itafungwa kesho kwa mchezo kati ya wenyeji Azam FC wakiikaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex.
Endapo Azam FC itashinda mchezo wa kesho itafikisha alama 25 na kuongoza ligi. Kwa upande wa Mtibwa Sugar ikishinda itafikisha alama 20 hivyo kuwa sawa na Singida United yenye alama 20 katika nafasi ya nne.