Simba, Tanzania Prisons Hapatoshi Leo Uwanja wa Sokoine

Simba, Tanzania Prisons Hapatoshi Leo Uwanja wa Sokoine
VINARA Simba kutoka Dar es Salaam wanatarajia kushuka dimbani kuwakabili Tanzania Prisons "Maafande" katika mechi ya raundi ya 10 ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika leo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini hapa.

Mabingwa hao wa Kombe la FA wanashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupata pointi tatu dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopita wakati wenyeji Tanzania Prisons wao walitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar ugenini Bukoba.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mechi hiyo ambayo itakuwa na ushindani na changamoto kutoka kila upande.

Omog alisema kikubwa katika mechi ya leo ni wachezaji wake kuwa makini na kutumia vyema nafasi watakazozitengeneza huku akiitaja safu  ya ulinzi ya Tanzania Prisons ni imara na imefanya vizuri katika mechi zilizopita.

Mcameroon huyo alisema pia anataka kila mchezaji atakayepangwa kucheza kwa bidii na kujiongezea nafasi ya kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho ambacho kiko kwenye mchakato wa kujiimarisha  kuelekea mashindano ya kimataifa hapo mwakani.

"Ni mechi ngumu kama nyingine zilizopita, najua timu za jeshi huwa imara na wachezaji wake huitaji mbinu za ziada kufikia ubora unaotakiwa, wana nguvu, wanapumzi nzuri, lakini nasi tumejipanga kuwakabili ili tutimize malengo," alisema Omog.

Amewaambia wachezaji wake kuwa wanadeni la kuhakikisha msimu huu wanapata pointi zote sita jijini hapa kutokana na kuwapokea vizuri katika mikoa yote ya jirani waliyokwenda kucheza mechi za kirafiki.

Wakati safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na Mganda Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya,  Mohammed Rashidi wa Tanzania Prisons mwenye mabao sita ndiye anatarajiwa kuibeba timu yake katika mchezo wa leo.

Mechi nyingine za ligi hiyo ya juu Tanzania Bara zitakazochezwa leo ni kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Ndanda FC, Njombe FC wao wataikaribisha Azam FC wakati Stand United itaivaa Mwadui na Majimaji watachuana na Mbao kutoka jijini Mwanza.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 itaendelea tena kesho kwa mabingwa watetezi kuwakaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na "ndugu" Mtibwa Sugar watacheza na Kagera Sugar huko Manungu, Turiani Morogoro.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad