BAADA ya kuishuhudia Yanga ikiichapa Mbeya City kwa mabao 5-0, hivyo kuzidi kupunguza wigo wa mabao dhidi yao, vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamepania kuibuka na ushindi mnono kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Lipuli ya Iringa, imeelezwa.
Simba inayodhaminiwa na Kambuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itakuwa mwenyeji wa Lipuli kwenye mchezo wao wa Jumapili utakaochezwa katika Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na klabu ya Azam.
Kocha Msaidizi wa Wekundu hao wa Mismbazi, Masoud Djuma, alisema baada ya michezo migumu ya mikoani, sasa wanaelekeza nguvu kwenye mchezo huo na lengo ni kuhakikisha wanapata ushindi mzuri ili kuendelea kukaa juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
“Ligi ni ngumu, unaona kila timu inajitahidi kupata ushindi, tupo juu ya msimamo kwa tofauti ya mabao ili kuendelea kufanya hivyo ni lazima tujitahidi kupata ushindi, lakini ushindi wa mabao mengi,” alisema Djuma.
Alisema baada ya michezo miwili ya mkoani Mbeya, kwa sasa nguvu zao wanazielekeza kwenye mchezo dhidi ya Lipuli huku wakijipanga kuhakikisha wanapata ushindi mnono.
“Tunaendelea na program yetu ya mazoezi…, tunajua kila mchezo utakuwa mgumu, lakini ni lazima tujipange na kujiandaa kupambana kwa ushindi hicho ndicho kitu cha muhimu,” aliongezea kusema.
Simba wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 22 sawa na Azam, lakini ikiizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Baada ya michezo ya mwishoni mwa wiki hii ikiwa ni mzunguko wa 11, Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kusimama kwa muda kupisha michuano ya Chalenji itakayofanyika Nairobi, Kenya.