Ubomoaji wa ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) unatarajiwa kuanza kufanyika baada ya mwezi mmoja.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi na Meneja wa Wakala wa Barabara Dar es Salaam (Tanroads), Julius Ndyamkama.
“Leo tutaweka alama ya X kwenye jengo la Tanesco kwa ajili ya kuanza ubomoaji. Baada ya kuweka alama ya X tutawapa notisi ili kuwajulisha kuhusu zoezi hilo,” amesema .
Hiyo ni baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo kwa wakala wa barabara nchini kubomoa jengo la Tanesco kupisha ujenzi wa mradi wa barabara za juu zinazotarajiwa kujengwa eneo la Ubungo jijini hapa.
Mradi huo mzima utaigharimu Tanzania kiasi cha Sh188 bilioni
Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati alipotembelea eneo la mradi huo mara baada ya kutua jijini Dar es Salaam akitokea Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Ubomoaji huo pia utahusisha ofisi za Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambazo pia zinapakana na jengo la Tanesco eneo la barabara ya Morogoro.