Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga inatarajia kuwaburuza mahakamani wawekezaji wakubwa kwenye migodi ya Madini ya almasi baada ya kushindwa kulipa kodi ya huduma ya jamii zaidi ya shilingi milioni 480 zilizotakiwa kulipwa tangu mwaka 2011 hadi mwaka huu wa 2017.
Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Steven Magoiga katika baraza la Madiwani baada ya kutokea sintofahamu katika taarifa ya fedha katika kipindi cha robo mwaka hali iliyomlazimu mkurugenzi kutamka wazi wazi juu ya mgogoro kati ya mgodi wa alimasi wa Mwadui na serikali kuwa umekuwa chanzo cha kuikosesha halmashauri ya Kishapu mapato na kuchangia kudidimiza miradi ya Maendeleo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu, Steven Magoiga amesema wawekezaji wa madini ya almasi na dhahabu wamekuwa wakikwepa kulipa kodi ya serikali hali iliyoilazimu TMAA kuchunguza na kubaini udanganyifu wa zaidi ya shilingi milioni 111 na kutoa taarifa kwa halmashauri kuwa fedha hizo ni lazima zilipwe kama kodi halali ya huduma.
Kwa upande mwingine mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu Bw. Boniface Butondo amesema wawekezaji wanaotuhumiwa wana nafasi moja ya kuketi pamoja na uongozi wa halmashauri kuweka mikakati ya kulipa deni hilo kabla ya kesi kufika mahakamani.