Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekubaliana kuhakikisha kundi la wapiganaji wanaojiita Islamic State (IS) wanashindwa nchini Syria, maafisa wa rais wa Urusi wamesema.
Ikulu ya Urusi imesema taarifa imeandaliwa na wataalamu baada ya viongozi hao wawili kukutana kwa muda mfupi pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za Asia na Pasific nchini Vietnam Jumamosi.
Kwa jumla, viongozi hao wawili walikutana mara tatu katika kipindi cha saa 24 katika mji wa Da Nang.
Hakujakuwa na thibitisho lolote rasmi kutoka kwa Marekani kuhusu tamko hilo la Urusi.
Mkutano kati ya Rais Trump na Vladimir Putin ulitarajiwa kufanyika wakati wa mkutano huo wa Apec, lakini ni maelezo machache sana ambayo yametolewa.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza Julai katika mkutano wa G20 katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani
Maswali kuhusu uhusiano wa Donald Trump na Urusi yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara.
Wasaidizi wake wakuu wa zamani wanachunguzwa kwa tuhuma za kushirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2016.
Ingawa White House haijasema chochote kuhusu mkutano wa wawili hao, taarifa ya Kremlin iliyotolewa Jumamosi imesema viongozi hao "waliafikiana kwamba mzozo wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi".
Kadhalika, walikariri "kujitolea kwao kuwashinda Isis [jina jingine la IS]" na kuzitaka pande zote kushiriki mazungumzo ya amani ya Geneva.
Trump na Putin 'Waafikiana Kuuwashinda Islamic State Nchini Syria'
0
November 11, 2017
Tags