Tundu Lissu Afunguka Mazito Hali Ilivyokuwa Siku ya Tukio la Kushambuliwa

Tundu Lissu Afunguka Mazito Hali Ilivyokuwa Siku ya Tukio la Kushambuliwa Kwake
 Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio na pia kueleza ujumbe aliompa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipomtembelea hospitalini jijini hapa juzi.

Mbunge huyo, ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, pia amesema amepitia majaribu mengi, lakini “hili ndilo kubwa”.

Amesema hali yake inaendelea vizuri na madaktari wanamuelezea kuwa ni “muujiza unaoishi” baada ya kufanikiwa kuunganisha vipande vya mwili ulioharibiwa kwa risasi.

Lissu alisema hayo alipofanya mahojiano na Mwananchi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha Tanzania tangu ashambuliwe.

Lissu amelazwa Hospitali ya Nairobi jijini hapa tangu Septemba 7 na huenda akahamishiwa nje ya bara la Afrika kwa matibabu zaidi, ambayo yatahusu mazoezi, kabla ya kurejea nchini.

Akizungumza na Mwananchi hospitalini hapo, Lissu alisema sasa anaamini kuwa Rais John Magufuli anajua kuna mgonjwa Nairobi na hivyo kufungua milango kwa wengine waliokuwa na hofu.

“Mimi namuamini na naendelea kuamini kwamba kwa sababu sasa Makamu wa Rais amekuja kwa niaba ya Rais, ametambua tuna mgonjwa yupo Nairobi. Milango itafunguka kwa wale wengine wote waliokuwa na hofu ya kuja,” alisema Lissu.

“Sasa Rais mwenyewe kamtuma makamu wake kuja kunipa pole, kwa hiyo hao wengine wa taasisi zote hawana hofu ya kuja kuniona.”

Akizungumzia mazungumzo yake na Suluhu, Lissu alisema yalikuwa mazuri.

“Mama Samia ni kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Tanzania pamoja na mihimili yake kuja kunitembelea,” alisema Lissu.

“Spika wa Bunge hajaja, katibu wake na uongozi mzima wa Bunge haujaja. Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi hawajaja pamoja na kwamba mimi ni Rais wa TLS.

“Na kwa kawaida mila na desturi za mahakama zetu, bila mawakili hakuna mahakama na kama Rais wa TLS nimekuwa nikialikwa na kuhudhuria vikao mbalimbali vya kiutendaji, lakini tangu nimeshambuliwa Jaji Mkuu au uongozi mzima wa Mahakama hata kutoa salamu za pole, hakuna.

“Rais Magufuli alikuwa hajawahi kusema lolote kuhusu kushambuliwa kwangu kama nakumbuka, lakini leo (juzi) amekuja Makamu wa Rais na amenieleza na napenda kuamini ni kweli ametumwa na Rais kama sehemu yake ya shughuli zilizomleta Kenya apitie kunisalimia na kunipa pole.”

Alisema Makamu wa Rais, ambaye waliwahi kufanya naye kazi wakati akiwa waziri anayehusika na Muungano na Lissu akiwa waziri kivuli wa eneo hilo, alimuuliza kama ana jambo lolote la kumweleza Rais, naye akamweleza kuhusu gharama za matibabu.

“Mimi bado ni mbunge, ujumbe ambao nataka aupeleke ni Bunge liko wapi? Bunge ambalo lina wajibu wa kisheria wa kunihudumia nikiwa naugua?” aliuliza Lissu akirejea mazungumzo hayo na Suluhu juzi jioni.

“Nilimpa ujumbe huo na napenda kuamini ataufikisha na ujio wake peke yake unatakiwa kufungua milango kwa wale waliokuwa wanafikiri wamefungiwa.”

Alisema suala la Bunge kuwa mbali naye ni mfano mwingine unaotia shaka kuhusu kushambuliwa kwake.

“Mimi ni mbunge na ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ninatambuliwa na Sheria za Tanzania, Sheria inayohusika ni ya uedeshaji wa Bunge. Sheria inaeleza kwamba mbunge anapoumwa atapata matibabu pamoja na gharama nyingine kutoka bungeni,” alisema.

Lissu alisema kila mbunge anayeumwa analipiwa gharama zote na Bunge na vile vile kama itabidi, alazwe nje ya Dodoma iwe Dar es Salaam, Afrika Kusini, India Marekani au Kenya.

“Analipwa posho na Bunge na mtu anayemuuguza analipwa posho vile vile, nusu ya posho ya mbunge ili kumudu gharama za maisha,” alisema.

“(Lakini) Tangu nimeumizwa, Spika anajua, alitangaza bungeni mbunge mwenzetu anaumwa. Tangu wakati huo mpaka leo Spika hajaja, Katibu wa Bunge, Tume ya Bunge haijaja,” alisema Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Alisema  kuna wabunge wawili CCM, Mary Chatanda (Korogwe Mjini) na  Fakharia Shomar Khamis (viti maalum na mmoja wa watumishi wa Bunge walifika siku ya Jumapili, siku ambayo si ya kazi.

“Walikuja kunipa pole, walikaa hapa wakanipa nipa pole, halafu wakaniaga. Nikawauliza mmetumwa chochote, wakasema hapana,” alisema.

“Nikamuuliza ofisa wa Bunge, ‘kuna ujumbe umetumwa uniletee, akasema hapana. Kwa hiyo hao wawili walikuja kibinafsi tu.

“Tume ya Huduma za Bunge inayoshughulikia mambo haya, haijaja mpaka leo. Kwa hiyo ukiachilia mbali matangazo ya Spika, Bunge halijaja kabisa, halijanishughulikia kwa lolote.

“Hakuna anayeomba fadhila, nataka haki, nitendewe haki, anayetendewa mbunge yoyote anayeumwa. Hakuna anayelilia fadhila hapa, hakuna anyeomba ufadhili. Nataka Bunge litimize wajibu wake wa kisheria. Hili nitalipigania, kama siwezi kudai haki yangu ya kisheria ambayo iko wazi, kama ya kwangu naona inakanyangwa kwa makusudi tu, nitapigania ya nani?”

Lissu alisema Bunge halina sababu za maana za kutomgharimia, bali ni kupiga chenga tu.

“Wameandikiwa barua na ndugu yangu mara hawajaiona, kwa hiyo lazima nipiganie haki yangu ili nipiganie haki za wengine,” alisema.

Niliona watu wawili wenye silaha

Katika mahojiano hayo na Mwananchi yaliyochukua takriban dakika 60, Lissu pia alielezea jinsi shambulio dhidi yake lilivyofanyika Septemba 7, lakini tofauti na kauli ya ndugu zake kuwa anawajua watu hao, alisema hawafahamu watu hao na kusisitiza suala la wachunguzi kutoka nje.

“Nilitoka bungeni muda wa saa saba hivi,” alisema.

“Kabla sijatoka nilichangia mjadala wa mkataba kati ya Malawi na Tanzania kuhusu Mto Songwe. Baada ya kumaliza kuzungumza nikakaa kidogo kisha nikatoka na kwenda nyumbani kwa chakula cha mchana.

Alisema alivyofika nyumbani, wakatokea watu eneo la kuegesha magari katika nyumba hizo za Serikali, ambako anaishi jengo moja na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), Dk. Haji Mponda na mmoja wa makatibu wakuu wa wizara.

“Kwa hiyo nakaa katika nyumba za Serikali. Watu wameingia katika nyumba za Serikali zinazolindwa saa 24, block inayotazamana na nyumba yangu, anakaa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na huwa kuna polisi nje saa 24,” alisema.

“Lakini watu wameingia wenye silaha, wakaja kunishambulia. Sikuwatambua kwa sababu nilishambuliwa nikiwa katika gari sikutoka nje. Dereva wangu aliniambia kuna watu wako nyuma wananifuata nisifungue mlango.”

Alisema alijaribu kuwaangalia kwa kutumia kioo cha pembeni ya gari na kuwaona watu wawili wakitoka na bunduki. Yaliyofuata nimekuja kujikuta nipo hapa nilipo leo wiki moja baadaye.

“Kwa hiyo, siwezi kusema ninawafahamu walionishambulia. Sikutambua hata mmoja wao ila najua nilishambuliwa na watu wawili katika gari iliyokuwa na vioo vyeusi.”

Lissu alisema wiki tatu kabla ya shambulio hilo alilalamika hadharani kwamba anafuatiliwa kila anapokwenda na siku moja aliwasimamisha watu hao katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro na kuwauliza sababu za kufanya hivyo.

“Niliwauliza kwa nini wananifuata na kama kuna mtu kawatuma, mwambieni mimi si mhalifu. Lakini sikupewa ulinzi wowote,” alisema.

Wachunguzi kutoka nje

Kama ilivyo kwa familia yake na Chadema, Lissu anataka uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na taasisi ya nje.

“Serikali inakosea sana,” alisema.

“Hili ni tukio la mbunge kushambuliwa akiwa maeneo ya Bunge. Kisheria hayo maeneo yanayoitwa ya Bunge ni pamoja na makazi ya wabunge wanapokuwa bungeni.”

Alisema huwezi kuwa bungeni kama huna sehemu ya kulala, kwa hiyo makazi yangu ni sehemu ya Bunge.

“Kitendo cha mbunge kushambuliwa wakati vikao vinaendelea-- na mbunge mwenyewe ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na anajulikana kwa kuikosoa Serikali mara nyingi kwa muda mrefu, inatia shaka,” alisema.

“Kitendo hicho peke yake kingetosha kutilia shaka uchunguzi wowote utakaofanywa na wale ambao mbunge huyo amekuwa akiwasema mara kwa mara. Kitendo hicho kingetosheleza kualika watu kutoka nje kuja kufanya uchunguzi.

“Wanakataa kwa sababu zao, tunaelekea miezi mitatu, polisi hawajasema wanamshuku nani. Hakuna mtuhumiwa hata mmoja halafu kuna jitihada kubwa imefanywa na Jeshi la Polisi kuzuia raia kumsaidia huyu mbunge.”

Alisema polisi imewazuia watu wasisali, wasimwombee Mungu apone, watu wasimchangie damu, kusiwe na dalili zozote za wazi za kumuunga mkono na huyu ambaye ameshambuliwa na watu wanasemekana hawajulikani.

“Kumekuwa na jitihada kubwa sana kuzuia watu wasimsaidie huyu kuliko kufanya upelelezi, hiyo inatoa picha kwamba bila uchunguzi huru ukweli hautajulikana, utafichwa na pengine ndivyo wanavyotaka,” alisema.

Akizungumza huku akisisitiza kwa mikono yake, Lissu alisema katika mlango wa Waziri Kalemani, kuangalia block ya Naibu Spika Dk Tulia, kuna camera za CCTV zinazofanya kazi Saa 24 hivyo kwa mtu yeyote ambaye yupo eneo hilo anaonekana, lakini akasema kuna vitu vinaashiria kuwa kunahitajika jicho la pili kuangalia hili.

Alipoulizwa nafasi ya Rais Magufuli katika suala hilo la uchunguzi, Lissu alisema: “Rais anaweza akitaka kuelekeza. Polisi ndio wenye mamlaka ya kiuchunguzi, waalike wataalamu kutoka nje.

“Haitakuwa mara ya kwanza, hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo na haitakuwa aibu ila ni namna nzuri zaidi ili kuondoa wingu lililotanda juu ya kushambuliwa kwangu, ukweli utajulikana na hiki kimya si kizuri.”

Lissu pia alizungumzia hali yake kiafya na matarajio yake.

“Nafikiri kiafya Lissu anaendelea vizuri na matibabu, hajapona bado lakini anaendelea vizuri, madaktari wanasema hali yangu inakuwa inatengamaa kila siku,” alisema.

“Huko tulikotoka ni kurefu zaidi kuliko tunakokwenda, vidonda vyote vya risasi vimepona, sina bandeji mwilini, sina bandeji kabisa. Maana yake vile vidonda vyote vilivyotokana na kupigwa risasi vimepoma.”

Hata hivyo, Lissu, ambaye chama na familia yake imesema ataenda kumalizia matibabu nje ya bara la Afrika, alisema bado hajajua ataruhusiwa lini, ingawa anajiona yuko katika hali nzuri.

“Madaktari hawajanipa muda, na nafikiri hawajanipa muda kwa sababu nzuri tu, majeraha niliyokuwa nayo nilipoletwa hapa, yalikuwa makubwa sana, madaktari wenyewe wamekuwa wakiniambia mimi ni muujiza unaoishi,” alisema.

“Kwa hali niliyoletwa hapa ni muujiza unaoishi. Kazi kubwa walioifanya ya kwanza ilikuwa kuhakikisha wanaokoa maisha na wameokoa maisha. Kazi ambayo inafuata ni kuniwezesha kurudi sasa katika hali yangu ya kawakida, kuweza kujitegema kimwili.”

Alisema madaktari wamemuwekea vyuma, wameunganisha mifupa.

Alisema mikono ilikuwa haifanyi kazi, lakini sasa anaweza kuichezesha na kula na kwamba tiba hiyo inachukua muda lakini tuko katika hatua ambayo si ya kuokoa maisha, bali ya kurudisha mwili katika hali ya kawaida.

“Kimawazo nafikiri sijabadilika sana, Lissu wa kabla ya Septemba 7 na Lissu wa leo kimsimamo wa kisiasa hajabadilika kabisa. Lazima tupiganie demokrasia, hiyo ndiyo salama yetu,” alisema.

“Tuwe na utawala wa kidemokrasia unaojali haki za binadamu, tuwe utawala wa sheria, tuwe na mfumo wa uongozi unaojali maisha ya wananchi, unaowajibika kwa wananchi au kwa wawakilishi wake na huu ni msimamo wangu unajulikana na bado uko vile vile.

Aadhimisha miaka 20 ya ndao wodini

Wakati akiendelea kutibiwa hospitalini hapo, jana Lissu na mkewe, Alicia walitimiza miaka 20 tangu walipofunga pingu za maisha Novemba 29, 1997 na kama kawaida walikuwa pamoja wodini.

“Mke wangu nikuzungumzieje?” alimuuliza.

“Kazi kwako,” Alicia alijibu.

“Mke wangu mpenzi anaishi kiapo chake tulipooana na kesho (jana) tunatimiza miaka 20. Tulipooana nilimsikia anasema ‘katika shida na raha’ nitampenda, nitafanya nini na nini’. Kwa hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” alisema Lissu huku Alicia akitabasamu.

“Katika miaka hii 20, tumepitia majaribu mengi sana, lakini hili ndilo kubwa kuliko yote na nafikiri kama ni mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu kabisa kwa sababu amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia anavyozungumza ana msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa.”

Lissu alisema Alicia “ni mke wa kweli, aliyekubali kuchukua majukumu ya kuwa mke”, na kwamba anajisikia faraja na furaha ya kipekee kuwa naye na angepende wawe pamoja miaka 20 mingine.

“Najisikia mwanamme mwenye bahati sana kuwa naye. Ni mwanamke wa kipee sana kuwa naye. Tumetoka mbali sana na hii miaka 20 imekuwa mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa naye,” alisema.

Alicia pia alikuwa na lake moyoni.

“Miaka 20 ni mingi, lakini nikifikiria kama ni juzi tu. Halafu nilikuwa sitaki kumkummbusha nilitaka kumfanyia ‘surprise (kumstua),” alisema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na kutabasamu

“Lazima niwe mkweli. Kuna miaka mingine alikuwa busy (na kazi nyingi), anasahau hata siku. Tundu ni mme wangu, kikubwa naweza kusema ni rafiki yangu wa karibu sana wa miaka mingi sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na smart. Tumekuwa tukiishi hivyo.”

“Ujumbe wangu, Tundu siku zote aendelee kuwa Tundu tu. Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe ni Tundu niliyemjua siku zote.”

Je, utagombea Urais 2020

Mbunge huyo wa Singida Mashariki hakutaka kuzungumzia uchaguzi wa mwaka 2020 na hata alipoulizwa kuhusu kugombea urais alistuka.

“Nafikiri huu ni mjadala unaohitaji kusubiri wakati mwafaka,” alisema.

“Si mjadala unaoweza kufanyika katika kitanda cha Hospitali ya Nairobi, Kenya. ni mjadala unaohitaji tukae, tushauriane. Kwa sababu ni chama lazima tukae tushauriane. Nafikiri hiki kitanda changu si mjadala wa kuanzisha, kama watu wananitajataja huko waendelee tu lakini mimi mjadala huu unisubiri nje ya hospitali.”Lakini Lissu alisema kwa sasa atakuwa wa tofauti kwa kuwa amepitishwa tanuru la moto na amepata uzoefu wa kutosha baada ya kujifunza mengi kutokana na tukio la Septemba 7.

“Nikitoka hapa kama Mungu amenipa pumzi ya kuendelea kuishi, haya mafunzo yatakuwa sehemu ya Lissu huyo baada ya Septemba 7. Nimejifunza kuwa Watanzania ni watu wa upendo sana. Pamoja na propaganda zote, uongo wote na ubaya wa watu, lakini Watanzania ni watu wa upendo sana,” alisema Lissu

“Wanafahamu nani anawapigania. Kuna rafiki yangu wa Dodoma ameniambia baada ya kupigwa risasi kuwa mji mzima ulihamia hospitali. Ingawa siku zote CCM wanashinda pale, siku hiyo walihamia pale (hospitali). Watanzania kila mahali walienda makanisani, misikitini, nafikiria huo upendo nitaulipaje.

“Nafikiria ni upendo ni kwa sababu ya kazi niliyoifanya bungeni na nje ya Bunge na hiyo kazi kama imewafanya wawe na upendo namna hiyo, basi nitaizidisha na nitawafanyia kazi iliyo bora zaidi.
Chanzo: Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad