Uchambuzi: Kama Urais Ungekuwa Wa Miaka Miwili..

Uchambuzi: Kama Urais Ungekuwa Wa Miaka Miwili..
Ndugu zangu,

Niliandika makala mara ile Rais John Pombe Magufuli alipotimiza Mwaka Mmoja akiwa madarakani.

Itakumbukwa, mwaka jana, na kwenye siku yake ya kuzaliwa, Rais wa Awamu ya Tano, Dr John Pombe Magufuli aliacha kula keki yake ya kusheherekea siku yake hiyo na kuamua kuwa kazini.
Zikatujia taarifa kubwa mbili katika siku hiyo; utenguzi wa uteuzi wa DCI na ziara ya kushtukiza wizara ya Maliasili na Utalii.

Niliandika, kuwa nataka niwe mkweli kwa nafsi yangu, kuwa hata kama tungekuwa, kama nchi, na utaratibu wa kuwa na Rais wa kipindi cha mwaka mmoja, basi, huyu tuliye naye sasa, John Pombe Magufuli, angekuwa amemaliza muda wake wa mwaka mmoja akiwa ameacha alama nyuma yake. Alama za kudumu muda mrefu.

Nikasema, kuwa ukweli nchi yetu imeanza kubadilika na fikra za watu wake pia zimeanza kubadilika. Maana, ilifika mahali, kuna walioacha kazi kwenye NGO- Mashirika yasiyo ya Kiserikali na kwenda kufanya kazi Serikalini ikiwamo kwenye Halmashauri zetu wakitamka wazi kuwa kwenye NGO kazi ni nyingi, wanarudi Serikalini na kwenye Halmashauri kupumzika na kula posho za safari na nyinginezo.

Nchi haiwezi kusonga mbele ikiwa na watu wenye mitazamo kama hiyo. Ni lazima kuwe na nidhamu ya utendaji kazi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu. Na wenye kukiuka hayo, ni lazima wajue kuna adhabu yenye kuendana na matendo yao maovu. Ndiyo siri kubwa ya nchi za wenzetu zilizoendelea.

Novemba 30, 2015 niliandika kwenye jarida la Raia Mwema, kuwa Magufuli ana uwezo wa kumwona bata na sungura kwa wakati mmoja.

Hii ni dhana kongwe ya kimtazamo iliyojengeka kifalsafa. Ni uwezo wa mwanadamu katika taswira moja kuwaona viumbe wawili wenye kufanana. Hivyo, inahusu uwezo wa kuliona jambo hilo hilo katika sura tofauti.

Ndio, kuna kuona kikiwa na kuona kama. Kuliangalia jambo kwa mtazamo tofauti.
Mwanafalsafa Thomas Kuhn yeye anazungumzia dhana ya ' Paradigm Shift'. Ni ile hali ya uwepo wa mapinduzi ya kifikra na ya kisayansi yenye kupelekea mabadiliko ya kimsingi katika jambo lile lile tulilokuwa na mazoea nalo.

Captain Thomas Sankara, kiongozi mwanapinduzi aliyeuawa wa Burkina Faso, katika wakati wake, alizungumzia umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kuyapa mgongo mazoea ya kale.

Sankara aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani. Mwanamapinduzi huyu alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso.
Sankara alipata kukaririwa akisema: “Ningependa kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi.

Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu. Hali hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa kuzipa mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali. Ni wendawazimu wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo. Ninataka kuwa mmoja wa wendawazimu hao.” (Hayati, Kapteni Thomas Sankara)
Yumkini tunachokishuhudia kwenye nchi yetu ni Magufuli's paradigm shift'. Hali ya kuwa na mabadiliko ya msingi.

Nimeona nini kwa Rais Magufuli baada ya miaka miwili?
Kama Urais ungelikuwa wa miaka miwili, basi, Rais tuliye naye, Dr John Pombe Magufuli, angeondoka akiwa ameacha alama chanya za kudumu milele.
Maana, akiingia mwaka wake wa pili, ninachoona ni upepo chanya wa Magufuli wenye kuendelea kuvuma, ndani na nje ya mipaka.

Huo ndio ukweli mwingine ningependa kuusema. Nimepata bahati ya kusafiri sehemu mbali mbali za nchi. Nimekuwa na mazoea ya kuzungumza na waananchi kupata mitazamo yao.
Mahali pengi kabisa, John Magufuli yumo kwenye midomo ya Watanzania wa kawaida walio wengi ikiwamo vijana ma-bayaye wanaoongezeka kwenye miji yetu.
Kwanini?

Naamini, John Magufuli amefaulu kufanya kile watangulizi wake hawakufaulu, ukimwacha Mwalimu. Magufuli sio tu amebeba ajenda ya vita dhidi ya ufisadi, rushwa na uhujumu uchumi, Magufuli anaifanyia kazi ajenda hiyo na watu wanaona ikifanyiwa kazi.
Ni kwa kiwango kile ambacho Hayati Sokoine alikuwa anakwenda nacho na akawa kipenzi cha umma.

Nimeandika huko nyuma, kuwa kero nambari moja kwa Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita ilikuwa Rushwa na Ufisadi, kero nambari mbili ilikuwa Rushwa na Ufisadi, na kero nambari tatu ni Rushwa na Ufisadi. Hivyo, hiyo ndio ilikuwa ajenda kuu.
Huko nyuma upinzani, tofauti na CCM, ndio ulibeba ajenda hiyo, wakaipoteza njiani, sasa upinzani unahangaika kutafuta ilichokuwa nacho.

Ndio maana, tofauti na huko nyuma, maeneo mengi nilimopita, huwezi sasa kuona tofauti za wananchi za kiitikadi, wote wanajadili ajenda moja, ya kupiga vita ufisadi na hali zote zenye kurudisha nyuma maendeleo yao. Wanamuunga mkono Rais John Magufuli. Hao ni Wana CCM na Wana- Chadema.

Jipya jingine ndani ya miaka hii miwili ni kitendo cha Rais Magufuli kuruhusu wananchi kutoa kero zao hadharani kwa kuandika kwenye mabango. Hali hii inaongeza uwajibikaji na kuwatia kiwewe viongozi warasimu na wenye kuwanyanyasa wananchi. Hawa huko nyuma walijificha kwenye risala kwa Rais ambayo ilikuwa na maana ya kumsomea Rais taarifa ya kumfurahisha na wananchi hawakuwa na pa kumsomea Rais risala inayotokana na wao wananchi. Siku hizi inawezekana kupitia mabango.

Wananchi wanamuunga mkono pia Rais Magufuli kwa nia yake ya dhati ya kusimamia rasilimali za taifa hata kuwa tayari kugombana na matajiri wamiliki wa makampuni makubwa ya uchimbaji madini.

Haijawahi kutokea wala kufikiriwa , kuwa, kama nchi, tungeweza kutunisha misuli na kufanikiwa kushinda kwenye meza ya majadiliano, kwenye kudai kipande kikubwa cha keki kwa maana ya kinachopatikana kutokana na uchimbaji wa madini yetu. Vita hivi vya kupigania rasilimali zetu. Vita hivi anavyoviongoza Rais John Magufuli vimemsogeza karibu zaidi kwenye mioyo ya wananchi ambao huko nyuma walianza kukata tamaa.

Kimataifa, Rais John Magufuli ametolewa mfano wa kuwa kiongozi mwenye kusimamia uwajibikaji. Nimepata kuongea na maafisa wawili waandamizi wa Balozi za Kimagharibi walioniambia wazi kuwa Rais Magufuli anafanya vema sana kwenye eneo la uwajibikaji na kukuza uchumi.
Mwingine akafikia kuniambia kuwa, haijawahi kutokea kwa Serikali ya Tanzania kurudisha fedha za misaada ambazo hazikutumika au zimepotea kutokana na ufisadi. Ndani ya miaka hii miwili, kwa mshangao wa afisa yule wa Ubalozi niliyeongea nae, ameniambia kuwa Balozi yao imepokea fedha ambazo Tanzania ilikuwa inadaiwa irudishe.
Nini tafsiri ya jambo hilo?

Kwa mujibu wa afisa yule wa Kibalozi, kubwa kabisa Serikali inayoongozwa na Magufuli sasa inaaminika na wahisani na mabenki yenye kukopesha. Kwamba kuna usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo. Kwamba sasa si rahisi fedha kuliwa na wajanja na kwamba zitafanya yale yenye kuwaletea wananchi maendeleo.

Nini siri kubwa ya hatua hii mpya? Nilimwuliza afisa yule wa Ubalozi;
" Ukiwa na Rais aliye juu na anayesimamia kwa vitendo yale yanayotakiwa kufanyika, basi, huku chini watendaji hubadilika haraka na kufanya kilicho sahihi na hata kuwa na hofu ya kufanya ufisadi." Alianiambia afisa yule wa Ubalozi.
Nini faida na hatari ya mafanikio haya ya Rais Magufuli ?
Kwa nchi, hii ni fursa pekee ya kuungana na kumkabili adui aliye mbele yetu na aliyetufikisha hapa tulipo. Waliotufikisha mahali ambapo akina mama na watoto wetu wakakosa dawa na huduma nyingine.

Wananchi wakakosa mabomba ya maji na mengineyo, huku wachache wakichota fedha za umma kwa rushwa na ufisadi.
Baada ya miaka hii miwili, hatusomi tena habari za ufisadi mkubwa ukifanyika kwenye halmashauri na kwengineko Serikalini.

Hatari ninayoiona mbele yetu ni pale tunapokuwa na Rais mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuongozi ndani ya Chama chake na Serikali. Rais anayekubalika na wananchi wengi.
Kwamba akitumia vema ushawishi huu, na kwa kutanguliza hekima na busara, nchi yetu itakuwa mfano katika bara hili, ikiwamo pia kuimarisha misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria.
Lakini, kama Rais mwenye haya, akaja akaota mapembe, basi, hapo itabaki kuomba majaaliwa ya maanani.

Maggid Mjengwa.
Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Naaam Swadaktaaa. Mwandishi kumbe umeliona hilo. Ukisikia Tanzania mpya ndio hiii. Tanzania mpya inakuja. Hongera sana Mueshimiwa ndugu Raisi Magufuri anaipenda sanaa nchi yake na watu wake kushinda kitu chochote kile ndio maana hapendi kuona nchi yake inaharibiwa na watu wachache sanaa. Alafu kupelekea walio wengi kuhangaika na kutabika. nchi kukosa mwelekeo na kudhalaulika katika ramani ya dunia. hongera sanaaa rais

    ReplyDelete
    Replies
    1. Jamani sisi wapinzani hatupendi kusikia hayo, tunafurahi kusikia serikali imekwama hapa imekwama pale, mnapozungumzia mafanikio mnatuumiza wenzenu, hebu msitufanyie hivyo, tunajitahidi kuivuruga serikali kwa maneno kila uchwao, tunahitaji maandamano ili tuitoe kwenye reli serikali na polisi wawe bize kutufuatilia, mengine yadode, kila tufanyayo hayaendi vile tunavyopanga, kwani kunani jamani? Tukimshambulia wahisani wanamkubali, Tumebanika mbele na nyuma, wapinzani wenzangu, kwani tumekosea wapi jamani....inatuuma sana

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad