Zaidi ya theluthi mbili ya watu wazima hupatwa na tatizo la kukosa usingizi. Tatizo hili huchangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuwa na msongo wa mawazo, wasiwasi na magonjwa mengine mbalimbali.
Tatizo la kukosa usingizi siku hizi linawakumba hata vijana wadogo ambao kwa nyakati za nyuma hatukuzoea kusikia wakiwa nalo.
Vyakula tunavyokula kabla ya kulala vimekuwa na mchango mkubwa katika kupata usingizi kwa muhusika.
Ili kuhakikisha kuwa unapata usingizi mwanana na mwororo unapolala, hakikisha kabla ya kwenda kulala umekula vyakula ambavyo vitachangia wewe kulala vyema.
Utafiti uliofanywa na Michael Grandner, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Arizona, Ndaki ya sayansi ya Afya umebaini kuwa vyakula vyenye wingi wa virutubisho vya ‘Tryptophan’ na asidi ya amino vinachochea mtu kupata usingizi kwani vinapoingia mwilini hubadilishwa na kuwa kemikali ya ubongo inayohusiana na usingizi.
Hivi ni baadhi ya vyakula ambavyo vitakusaidia kupata usingizi murua.
Mayai ya kuchemsha
Kama huwa unapata shida ya usingizi ama hupati usingizi wa kutosha, basi inawezekana ni kwa vile huli vyakula vyenye wingi wa protini. Kula vyakula kama vyenye utajiri wa protini kama vile mayai ya kuchemsha, siagi, karanga na vinginevyo vingi, havitakufanya tu kupata usingizi, bali utakuwa na usingizi mnono na wa muda mrefu.
Maziwa
Maziwa yana virutubisho vya ‘tryptophan’ ambavyo vina mchango mkubwa sana katika kukupa usingizi mwanana. Siyo hivyo tu, maziwa yana utajiri wa madini ya ‘Calicium’ ambayo husaidia katika kuondoa wasiwasi na msongo wa mawazo. hivyo kukufanya ulale pasipo na mawazo yoyote yanayokusumbua.
Ndizi mbivu
Kama umehangaika kupata usingizi, basi unashauriwa kutumia tunda la ndizi kabla ya kulala. Ndizi ina wingi wa madini ya ‘magnesium na potassium’ ambayo huihuisha misuli. Vilevile ina virutubisho vya ‘tryptophan’ ambavyo hukufanya kuwa na usingizi mwororo. Ukipata mchanganyiko wa ndizi na maziwa basi usiku wako utakuwa murua zaidi.
Samaki
Samaki huwa na wingi wa vitamini B6 ambavyo hutumika kutengeneza melatonin (homoni ambayo huchochea usingizi wakati wa usiku.)