Wanafunzi 6 wa Chuo Kikuu UDSM Watimuliwa kwa Utovu wa Nidhamu

Wanafunzi 6 wa Chuo Kikuu UDSM Watimuliwa kwa Utovu wa Nidhamu
Wanafunzi sita kati ya 100 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliokuwa kwenye mpango wa mafunzo ya vitendo kwenye taasisi na kampuni mbalimbali wameondolewa kwenye mpango huo kutokana na utovu wa nidhamu.

Mpango wa majaribio ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa UDSM unatekelezwa na Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (Taesa) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Akizungumza leo Ijumaa Novemba 17,2017 wakati wa kikao cha tathmini, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taesa, Boniface Chandaruba amesema baadhi ya wanafunzi hao hawajitambui na hawaoni umuhimu wa mafunzo hayo.

Amesema kati ya wanafunzi hao sita, baadhi waliwatukana wasimamizi wa programu hiyo na wengine kuwarekodi viongozi wao na kuwaweka kwenye mitandao.

"Wanafunzi wa aina hii hatutawavumilia tunawaondoa kwenye programu hii," amesema.

Amesema programu hiyo inawawezesha wanachuo kwenda kufanya mafunzo kwenye taasisi za Serikali, mashirika ya umma na kampuni binafsi ili kupata ujuzi na maarifa ya kazi wanazosomea.

Amesema sababu za kuanzisha programu hiyo ni kutokana na baadhi ya waajiri kulalamika kwamba wamekuwa wakiajiri wahitimu wa vyuo vikuu ambao hawajui kazi.

"Baadhi ya waajiri wanasema wanatoa ajira kwa watu ambao wanatakiwa kufundishwa kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja," amesema.

Amesema wanachuo hao wataendelea na mafunzo kwa miaka mitatu watakayokuwa chuoni.

"Wakifanya kazi vizuri na kuwavutia waajiri wanaweza kuajiriwa moja kwa moja watakapomaliza masomo," amesema

Mshauri wa Wanafunzi wa UDSM, Paulina Mabuga amesema licha ya wanafunzi hao kuondolewa katika mpango huo, pia uongozi wa chuo utachukua hatua za kinidhamu.

Ameipongeza Taesa na ILO kuanzisha mafunzo hayo kwa vitendo na kuichagua UDSM kuwa chuo cha kufanya majaribio.

Amependekeza mpango huo uwe endelevu ili kuwapa wahitimu uzoefu wa kazi wanazosomea.

Mmoja wa wanafunzi, Adelaide Mwasyoghe amesema anafanya mafunzo kwa vitendo katika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Amesema kwa muda mfupi ameweza kujifunza kazi na kufahamiana na wafanyakazi wenzake.

"Nikimaliza masomo sitahitaji kuelekezwa kwa sababu nitakuwa nafahamu mazingira ya kazi ya  kampuni," amesema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad