Watanzania wawili wamekamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi katika eneo la isiolo nchini Kenya, wakienda Somalia ambako wanahisiwa wakienda kujiunga na Al- Shabaab
Mkuu wa polisi kituo cha Isiolo Charles Ontita amesema Watanzania hao walikamatwa na maaskari katika bara bara ya Isiolo – Moyale karibu na njia panda inayoelekea Garba, na baada ya kuwapekua ndipo walibaini walikuwa Watanzania na hawakuwa na vibali vya kusafiria.
“Maaskari waliokuwa doria walisimamisha basi na kuanza kukagua, ndipo walipowakuta wageni wawili ambao hawakuwa na vibali, waliwaambia askari kuwa walikuwa wanaenda Moyale kufanya kazi ambayo wameitiwa, na baada ya kupekua simu zao walikuta baadhi ya namba za Somalia ambazo walikuwa wakiwasiliana nazo, na kusema ndio watu waliowaitia kazi”, amesema Kamanda Ontita.
Watanzania hao wametajwa kuwa ni Juma Abbas Zuberi mwenye miaka 28 na Ali Juma Kaondo wa miaka 17, wamepelekwa katika kituo cha polisi cha Isiolo, huku wakiendelea kuchunguzwa na Akskari hao wa kupambana na ugaidi kutoka Nairobi.