Walichimba njia hiyo kwa miezi kadha.
Polisi wameambia BBC kwamba pesa taslimu pamoja na vito vya thamani isiyojulikana viliibiwa.
Maafisa wanaamini kwamba wezi hao walikodisha chumba karibu na Benki ya Baroda kuwawezesha kuchimba njia hiyo.
Wanadaiwa kuendesha biashara ya kuuza mboga na matunda katika kiduka chao kuficha mipango yao.
Wezi hao walitoweka tangu Jumamosi usiku baada ya kutokea kwa wizi huo.
Haijabainika ni vipi wanaume hao walifanikiwa kuchimba njia hiyo kwa miezi kadha bila kugunduliwa.
Vyombo vya habari nchini India vimezungumza na wateja wa benki hiyo ambao vitu vyao vya thamani viliibiwa.
"Akiba yangu yote ilikuwa imewekwa kwenye sefu. Vito ambavyo tumemiliki kwa vizazi kadha, vimeibiwa," Dagdu Gavani, mmoja wa wateja aliambia Mumbai Mirror.
Wafanyakazi wa benki hiyo iliyo viungani mwa mji wa Mumbai waligundua wizi huo Jumatatu na kuwafahamisha polisi.
Polisi wameambia BBC kwamba sefu 30 kati ya 225 kwenye benki hiyo ziliporwa.
Washukiwa bado hawajatambuliwa.