Ni katika kuongoza safu ya ushambuliaji katika mechi dhidi ya Prisons, Tshishimbi bado...
HAKUNA kulala, hiyo ni kauli ya Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina kuelekea katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons itakayofanyika leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Yanga watashuka katika mechi ya leo wakiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City wakati wageni Tanzania Prisons wao wanaugulia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa vinara Wekundu wa Msimbazi.
Endapo Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa itapata ushindi leo, itaiondoa kileleni Simba ambayo pia inadhaminiwa na kampuni hiyo ambayo ilianzia Kenya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Lwandamina, alisema kuwa amewaandaa wachezaji wake kupambana kwa ajili ya kupata ushindi na kuwasisitiza waongeze umakini katika mchezo wa leo.
Lwandamina alisema hakuna mechi rahisi na amewaambia wachezaji wake wasifikirie ushindi mnono walioupata katika mchezo uliopita.
"Tuko tayari kwa mechi ya kesho (leo) Jumamosi, hii ni timu nyingine, sitaki wachezaji wangu wafikirie matokeo yaliyopita, hii haitawasaidia kwa sababu tunaingia kupambana na timu nyingine, tunahitaji kuwa na nguvu na mipango imara," alisema Mzambia huyo.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia gazeti hili kuwa wanatarajia straika wao Amissi Tambwe kucheza mechi yake ya kwanza msimu huu, lakini wataendelea kumkosa kiungo, Papy Tshishimbi ambaye enka yake imevimba.
Naye Kocha wa Singida United, Hans van der Pluijm, amesema kuwa anaamini kikosi chake kitaendelea kufanya vizuri wakati leo watakapoikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida.
"Tuko tayari, kila siku tunajiandaa ili tuwe imara kupambana kusaka pointi tatu, tunaamini na tunastahili kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani," alisema Mholanzi huyo.
Mechi nyingine za ligi hiyo ya juu nchini zinazotarajiwa kufanyika leo ni kati ya Mbao FC dhidi ya Mwadui wakati Kagera Sugar wataikaribisha Stand United na Ruvu Shooting watawaalika Majimaji ya Songea.