SIKU chache baada ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusema kuwa Tanzania Bara itashiriki michuano ya Chalenji itakayofanyika nchini Kenya, uongozi wa Yanga umedai kuwa michuano hiyo itawavurugia mipango yao waliyojiwekea kwa ajili ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Michuano ya Chalenji ambayo hushirikisha timu za taifa za nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), imepangwa kuanza Novemba 25 huko nchini Kenya.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema wao walikuwa wamejipanga kwa kuzingatia ratiba ya awali ya ligi kuu ambayo ilikuwa haionyeshi kama kutakuwepo na mashindano ya Chalenji.
“Ligi inaposimama kila wakati hakika inatuvurugia mipango yetu ambayo tulikuwa tumejiwekea kwa ajili ya kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu.
“Kama walijua kabisa kuwa safari hii tutashiriki michuano ya Chalenji walipaswa kutujulisha mapema katika ratiba ligi kuu kabla ya kuanza kwa ligi ili tuweze kupanga mikakati yetu tukijua kuwa itakapofika tarehe fulani kutakuwa na hiki siyo kutukurupusha namna hii.
“Wanatuvurugia mipango yetu lakini pia wanatuongezea gharama za uendeshaji wa timu, kwa sababu katika muda huo ambao ligi itakuwa imesimama tutalazimika kuiweka timu kambini kwa muda mrefu kitu ambacho hakikuwa kwenye mipango yetu,” alisema Mkwasa.