UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema haifurahishwi na kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusimamisha mechi za Ligi Kuu Bara ili kupisha michuano ya Kombe la Chalenji na kuongeza kuwa uamuzi huo "unaua" morali ya timu na kuwapa hasara.
Bodi ya Ligi Kuu imetangaza kuwa Ligi Kuu itasimama baada ya michezo ya raundi ya 10 ili kutoa nafasi kwa timu ya Tanzania Bara
"'Kilimanjaro Stars" kupata nafasi ya kujiandaa na kushiriki michuano ya Chalenji ambayo itaanza kufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 9 mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.
Akizungumza baada ya mazoezi ya jana asubuhi ambayo alihudhuria, Katibu Mkuu huyo wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema kusimama kwa ligi huyo kutawaathiri na kutapunguza morali ya wachezaji wake ambao tayari imeimarika.
"Kuna haja ya kuliangalia upya jambo hili, TFF inapopanga ratiba ya ligi iangalie na matukio kama haya, inapaswa timu kujua mapema ratiba hii, kusimama kwa ligi si vizuri, hata ligi yenyewe inakosa msisimko," alisema Mkwasa.
Kocha huyo wa zamani wa Yanga, Ruvu Shooting na Twiga Stars, alisema kuwa ana uhakika kusimama kwa ligi hiyo kutaziathiri pia timu nyingine na si Yanga peke yake.
Alisema itawalazimu kuwapa mapumziko wachezaji wao ambao hawatakuwa kwenye vikosi vya timu za taifa kama Kilimanjaro
Stars (Bara) au Zanzibar Heroes mpaka pale mashindano hayo ya Kombe la Chalenji yatakapomalizika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, aliiambia Nipashe jana kuwa wamelazimika kuisimamisha ligi baada ya TFF kuthibitisha kuwa mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kushirikisha nchi 12.
“Wakati tunapanga ratiba ya ligi kuu, Cecafa walikuwa hawana uhakika wa kufanyika kwa mashindano haya, ndio maana hatukuweka kwenye kalenda yetu, kwa bahati mbaya au nzuri mwaka huu yanafanyika kwa hiyo ilikuwa lazima tufanye hivi,” alisema Wambura.
Wakati huo huo, Mkwasa, alisema kuwa hana habari ya kutokuwapo nchini kwa mshambuliaji, Donald Ngoma, ambaye amekwenda kwao Zimbambwe kwa ajili ya kupata matibabu.
“Mimi sifahamu, Ngoma alikuja ofisini kwangu kuomba ruhusa ya kwenda kwao kupata matibabu ya majeraha yake, lakini nilimwambia anatakiwa kwanza azungumze na kocha na meneja wa timu kabla ya kuja kwangu, lakini nimesikia kaondoka,” alieleza Mkwasa.